News
Kikao cha Kusafisha eneo la Owino Uhuru Chachukua Mkondo tofauti
Mamlaka ya Mazingira nchini NEMA imefanya kikao na waathiriwa wa sumu ya Lead kutoka kijiji cha Owino Uhuru eneo bunge la Jomvu kaunti ya Mombasa ili kuwaeleza jinsi zoezi la kusafisha mazingira litakavyotelekelezwa katika kijiji hicho.
Kikao hicho kilichofanyika katika mtaa wa mataa ya ndege na wala sio eneo la Owino Uhuru kama ilivyoratibiwa awali kutokana na sababu za kiusalama, idadi ndogo ya wakaazi ndiyo waliyojitokeza kuhudhuria kikao hicho.
Akizungumza wakati wa kikao hicho, Mkurugenzi wa uzingatiaji na utekelezaji katika Mamlaka ya NEMA Robert Orina amekanusha madai yaliyoibuliwa kwamba mda uliyopewa Mamlaka ya NEMA wa kusafisha mazingira umepita, akiwataka wakaazi kushirikiana na mamlaka hiyo.
Kwa upande wake Mwakilishi wadi ya Mikindani kaunti ya Mombasa Jackton Madialo amewataka wakaazi kujiepusha na propaganda, na badala yake kuhakikisha wanaipa Mamlaka ya NEMA nafasi ya kusafisha mazingira ya Owino Uhuru.
Hata hivyo wakaazi waliohudhuria kikao hicho wakiongozwa na Samuel Obwaka wameeleza kuridhishwa na hatua ya NEMA kusafisha eneo hilo, wakiwataka wenzao kushirikiana na NEMA kutekeleza zoezi hilo.