News

KESSHA: Huenda shule za upili zikafungwa kufuatia ukosefu wa fedha

Published

on

Katibu Mkuu wa Muungano wa walimu wakuu wa shule za upili nchini KESSHA Abdinoor Haji
ameonya kuhusu uwezekano wa shule kufungwa mapema iwapo pesa za kugharimia masomo hazitatolewa haraka.

Haji alisema ukosefu wa fedha hizo umeathiri shughuli mbalimbali shuleni kote nchini.

Haji alisema ucheleweshwaji wa kutolewa kwa fedha hizo umesababisha viwango vya elimu kudorora na ndio chanzo kikuu cha upatikanaji wa alama za E katika mitihani ya kitaifa ya KCSE kwa muda wa miaka mitatu iliyopita.

“Shule za kutwa ndizo ziliathiriwa zaidi kwa sababu zinategemea pakubwa fedha hizo za serikali. Ukosefu wa fedha hizo umedumaza uwezo wa kufanikisha upatikanaji wa elimu bora,” alisema Haji.

Aidha, alisema kutokana na ukosefu wa fedha, shule nyingi zimeshindwa kuwalipa wasambazaji bidhaa huku baadhi ya shule zikilazimika kuwaachisha kazi walimu walioajiriwa na bodi za usimamizi wa shule.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa KESSHA Willy Kuria alisema shule za upili zinaidai serikali kuu shillingi bilioni 17 za muhula wa kwanza na wa pili.

Kuria alisema ikiwa Wizara ya Elimu nchini itakosa kulipa malimbikizi hayo ya madeni, shule zitalazimika kufungwa mapema kwa sababu ya ukosefu wa pesa za kuwaweka wanafunzi shuleni.

Taarifa ya Janet Mumbi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version