News
KEMNAC Yamtaka Rais Ruto Kufutilia Mbali Japo la Uteuzi wa Makamishna wa Wakfu wa Waislamu
Mwenyekiti wa baraza kuu la mashauri ya kiislamu nchini KEMNAC Sheikh Juma Ngao, amemtaka Rais William Ruto kulifutilia mbali jopo ambalo liliteuliwa siku chache zilizopita la kuwasajili Makamishna wa Tume ya Wakfu ya kulinda mali ya Jamii ya Waislamu nchini.
Akizungumza katika kaunti ya Mombasa, Sheikh Ngao amesema wale ambao waliteuliwa ili kutekeleza majukumu hayo hawana maadili na kwamba ni wabinafsi.
Sheikh Ngao amesema makamishna hao hawatakuwa na manufaa yoyote kwenye tume hiyo katika kulinda mali ya waislamu nchini kutokana na kwamba mali za jamii ya waislamu zinapaswa kulindwa vilivyo.
Ngao pia amesema tume hiyo imekuwa ikikumbwa na changamoto mbalimbali kutokana na kile ambacho anadai kuchangiwa na uteuzi ambao unatekelezwa kupitia njia ambazo hazifai.
Ikumbukwe kwamba siku chache zilizopita Mwanasheria mkuu nchini Dorcas Oduor aliwateua viongozi watano wa dini ya Kiislamu ili kuunda jopo ambalo litawasajili makamishna wa tume hiyo ya Wakfu inayosimamia mali ya jamii ya Waislamu nchini, licha KEMNAC kupuuzilia mbali jopo hilo ikisema halifai.