News
Kanisa la Kianglikana lawaonya wanasiasa dhidi ya ufisadi
Kanisa la Kianglikana nchini limejitokeza na kukemea kukithiri kwa sakata za ufisadi nchini katika Wizara mbalimbali likisema tabia hiyo inashusha hadhi ya taifa la Kenya.
Kanisa hilo limewakata wanasiasa kuchukua jukumu la kukabiliana kikamilifu na sakata za ufisadi nchini, likisema inachukiza kuona fedha nyingi za umma zikiporwa na baadhi ya watu wakati wakenya wanahitaji maendeleo.
Viongozi wa kidini wa Kanisa hilo wakiongozwa na Askofu wa Dayosi ya Mumia Joseph Wandera waliwakashfu viongozi wa kisiasa kwa kukosa kuwa waaminifu na kuchangia taifa kushuhudia ufisadi.
Viongozi hao aidha walisema ufisadi kwenye mamlaka ya afya ya jamii nchini SHA umekithiri zaidi na huenda ukasababisha wakenya wengi wakakosa huduma muhimu za afya nchini.
Viongozi hao wa kidini walishinikiza hatua za haraka kuchukuliwa za kukomesha sakata za ufisadi nchini sawa na kuwataka viongozi wa kisiasa kuhakikisha wanajitenga na ufisadi na badala yake kuwa mstari wa mbele kukomesha ufisadi.
Wakati huo huo waliwataka wanasiasa kujitenga na kampeni za siasa za mapema na badala yake kuangazia masuala ya maendeleo ili kuwahakikisha wananchi wananufaika kikamilifu na raslimali zilizopo nchini.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi