Sports
Aryna Sabalenka alimshinda Amanda Anisimova na kutetea taji lake la US Open siku ya Jumamosi
Mchezaji Nambari moja duniani mchezo wa tenisi kwa akina dada Aryna Sabalenka alimshinda Amanda Anisimova na kutetea taji lake la US Open siku ya Jumamosi, baada ya kumbwaga mpinzani wake Mmarekani kwa seti mbili mfululizo na kujinyakulia taji lake la nne la Grand Slam katika taaluma yake.
Sabalenka alitumia kwa ustadi udhaifu wa Anisimova kwenye huduma yake na kukamilisha ushindi wa 6-3, 7-6 (7/3) kwenye uwanja wa Arthur Ashe, ushindi uliothibitisha nafasi yake kama kinara wa tenisi ya wanawake duniani.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 27 kutoka Belarus aliingia kwenye fainali ya Jumamosi akijua hiyo ndiyo nafasi yake ya mwisho mwaka 2025 kushinda taji la Grand Slam, baada ya kupoteza kwenye fainali za Australia Open na French Open. Sabalenka alifuta makosa hayo kwa ushindi huu, na kuvunja ndoto za Anisimova za kupata ukombozi wa kipekee miezi miwili tu baada ya kupokea kipigo cha 6-0, 6-0 kutoka kwa Iga Swiatek kwenye fainali ya Wimbledon.
“Ni jambo la ajabu, masomo magumu yote yalistahili kwa ajili ya ushindi huu,” alisema Sabalenka baada ya kuwa mwanamke wa kwanza kutetea taji la US Open tangu Serena Williams mwaka 2014. “Sina maneno kwa sasa.”
Anisimova alikuwa ameshinda mechi sita kati ya tisa zilizopita dhidi ya Sabalenka, ikiwemo ushindi katika nusu fainali ya Wimbledon. Lakini Sabalenka, aliyekuwa akicheza fainali yake ya saba ya Grand Slam, alitumia uzoefu wake kikamilifu na kumaliza kabisa matumaini ya Anisimova ya kushinda taji lake la kwanza la Grand Slam.
“Kupoteza fainali mbili mfululizo ni jambo kubwa lakini pia gumu sana,” alisema Anisimova. “Nadhani leo sikupigania ndoto zangu vya kutosha,” akifichua kuwa mwanga chini ya paa lililofungwa uliathiri huduma yake.