Mahakama ya Kilifi imeagiza kukamatwa kwa washukiwa watatu akiwemo Wakili Devison Liano Kazungu, ambaye amekuwa akihudumu bila vibali halali pamoja Karani wake Hersi Mathius Kahindi na Lawrence Menza Gona ili wafikishwe Mahakamani.
Hii ni baada ya mshukiwa Charo Kazungu Baya kufikishwa Mahakamani pekee huku wenzake wakiwa mafichoni kufuatia kesi ya mauaji ya Silvia Panganin ambaye ni rais wa Uswizi.
Hakimu wa Mahakama hiyo Charles Obulutsa alitoa agizo hilo baada ya Afisi wa polisi anayechunguza kesi hiyo Felix Odwiya kuiambia Mahakama kwamba uchunguzi wa kesi hiyo bado unaendelea.
Mawakili wa washukiwa walimtea mteja wao na kuwasilisha ombi la kutaka aachiliwe kwa dhamana ombi ambalo limepingwa vikali na upande wa mashtaka ukiongozwa na Ridhwan Mohammed.
Katika kesi hiyo mshukiwa Charo Kazungu Baya alibainika kwamba mnamo mwezi Juni mwaka 2024 katika Ofisi za usajili wa ardhi mjini Kilifi alijisajili kama mmiliki wa kipande cha ardhi nambari gede/dabaso 454 yenye thamani ya shilingi milioni 26, mali ya marehemu Silvia Panganin, akisema alikuwa ameachiwa kama urithi.
Mshukiwa Baya anakabiliwa na shtaka lengine la kuchukua na kujisajili kama mmiliki wa gari aina ya Toyota Wagon nambari ya usajili KBU 076N mali ya Luigi Paganin yenye thamani ya shilingi laki tano na elfu hamsini, akisema aliuziwa na bibi yake marehemu Silvia Vera Panganin.
Kesi hiyo itaendelea mnamo tarehe 6 mwezi Machi mwaka huu ambapo Mahakama itatoa uamuzi wa ombi la kuachiliwa kwa mshukiwa kwa dhamana au la.
Taarifa ya Teclar Yeri
