News
IEBC kufanikisha chaguzi ndogo
Taifa sasa linajiandaa kwa chaguzi ndogo hasa baada ya kuapishwa kwa mwenyekiti na makamishna wapya sita wa tume ya uchaguzi na mipaka nchini IEBC hivi majuzi.
Chaguzi hizo zitatumika kutathmini ushawishi wa kisiasa kati ya rais William Ruto, waziri mkuu wa zamani Raila Odinga, aliyekuwa naibu rais Rigathi Gachagua na kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka.
Miongoni mwa maeneo kunakotarajiwa kufanyika uchaguzi mdogo ni eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi ambako wakaazi wamekuwa bila uwakilishi bungeni baada mahakama ya upeo kubatilisha ushindi wa Harrison Kombe kama mbunge wa eneo hilo mwezi Mei mwaka 2025.
Maeneo mengine ni Kaunti ya Baringo, eneo bunge la Banisa, Ugunja, Malava, Mbeere kaskazini na Kasipul.
Maeneo 15 ya uwakilishi wadi nchini pia wananchi watashiriki uchaguzi mdogo kutafuta wawakilishi wao wa wadi.
Chaguzi hizi zinatokana na hatua ya kuteuliwa kwa wawakilishi wa baraza la mawaziri nchini, baadhi ya viongozi kufariki, na kubatilishwa kwa matokeo ya uchaguzi wa baadhi ya wabunge na wawakilishi wadi kadhaa wa mabunge ya kaunti.
Taarifa ya Joseph Jira