Uhasama wa muda mrefu kati ya mastaa wakubwa wa rap, Cardi B na Nicki Minaj, umeibuka tena, ukifufua moja ya bifu maarufu zaidi katika historia ya hip-hop.
Drama hii imehamia mitandaoni baada ya Nicki kuonekana akikejeli albamu mpya ya Cardi Am I the Drama? huku akitoa kauli zenye kugusia ujauzito wake.
Nicki Minaj, mwenye umri wa miaka 42, amezua utata baada ya kushiriki meme kwenye akaunti yake ya X akiwa ameambatanisha na maneno ya kitata: “Raw doggin pregnant wit dat 4th babeeee Barney B. BV. HPveeeeeee Allegedlyyyyyy.”
Cardi B, mwenye umri wa miaka 32, hakupoteza muda kujibu mashambulizi. Katika posti yake, alimshutumu Nicki kwa kuendelea kuzungumzia ujauzito wake mara kwa mara huku akimkejeli pia kuhusu changamoto zake za kupata mtoto.
“Sawa basi, sasa hii ndiyo tweet ya tatu unayoongelea kuhusu ujauzito wangu… kama vile hukua ukihangaika kutoka kliniki moja ya fertility hadi nyingine kwa sababu huwezi kuzaa, eti mayai yako yaliharibika kwa sababu ya hizo dawa ulizokua unatumia. Sio ‘allegedly’… Mungu walinde watoto wangu,” Cardi aliandika.
Baada ya hapo, aliongeza pigo lingine akimkemea Nicki kwa kulinganisha kazi zao moja kwa moja:
“Kwa nini unaendelea kuzungumzia albamu yangu?? Uko kwenye muziki miaka 16 sasa. Unatakiwa ujilinganishe na wenzako—Rihanna, Taylor Swift, Drake. Hao ndio namba zako za kushindana nazo. Mimi nilikua bado sekondari ulipoanza. Kwa nini unajilinganisha na mimi??”
Kwa kuweka bifu hili kwenye msingi wa tofauti ya vizazi, Cardi alimuweka Nicki kama aliyeachwa nyuma kwa kung’ang’ania kulinganisha mafanikio yao licha ya kuanza safari zao katika vipindi tofauti.
Hii si mara ya kwanza wawili hawa kugongana. Tensi kati yao ilianza mwaka 2017 baada ya Cardi kung’aa kimataifa kupitia Bodak Yellow, jambo ambalo wengi waliliona kama tishio kwa ushawishi wa Nicki.
Mabishano yao yaliwahi kufikia kilele mwaka 2018 katika New York Fashion Week walipoingia kwenye ugomvi wa moja kwa moja. Tangu hapo, wamekuwa wakirushiana maneno makali kupitia mahojiano, muziki, na mara kwa mara mitandaoni.
Kama ilivyotarajiwa, bifu hili limegawanya tena mashabiki wao. Mashabiki wa Nicki, wanaojulikana kama Barbz, na wale wa Cardi, Bardi Gang, wamefurika kwenye majukwaa kama X na Instagram wakipiga hashtags, memes na mijadala mikali.
Wakati baadhi ya mashabiki wakitoa wito wa umoja kati ya wakali hawa wawili wa rap, wengine wanasisitiza kwamba kurushiana maneno huku ndiko kunakoipa rap uhai na ushindani.
Kwa sasa, Nicki bado hajajibu moja kwa moja mashambulizi ya Cardi. Lakini kutokana na historia yao ya makabiliano ya muda mrefu, mashabiki wanasubiri drama zaidi katika siku zijazo.
Kwa muda huu, mgongano wao unasalia kuwa kumbusho la jinsi bifu za mizani kubwa zinavyoendelea kuunda tasnia ya hip-hop—ambapo migongano binafsi mara nyingi huibuka hadharani, ikichochea mijadala, mgawanyiko, na vichwa vya habari duniani kote.