Msanii wa bango, Bavyombo, amezua gumzo kubwa kwenye mitandao ya kijamii baada ya kutangaza marufuku ya matumizi ya kauli maarufu “Mama Amina” ndani ya bendi yake ya Hosini Band.
Kupitia ukurasa wake wa Facebook, Bavyombo aliweka wazi kuwa kauli hiyo, ambayo imekuwa ikihusishwa mara nyingi na matamshi ya matusi na lugha chafu, haitavumiliwa tena katika bendi yake.
“HUKU HOSINI BAND ‘MAMA AMINA’ MARUFUKU KABISA,” aliandika Bavyombo kwa herufi kubwa, akionesha uzito wa msimamo wake.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo bandi tofauti za bango zimekuwa zikitumia kauli hiyo ambayo kiitikio chake ni matusi yasiyoandikika.
Mashabiki Wagawanyika
Baada ya chapisho hilo, mitandao ililipuka kwa hisia mseto. Wapo waliounga mkono hatua ya Bavyombo wakisema ni njia ya kurejesha heshima ya muziki, huku wengine wakiona ni kuchezea uhuru wa ubunifu.
Emmanuel Blait aliandika:
“Kazi ni kuharibu nyimbo ya mzee Ngala ya Mama Amina mkaweka ya matusi… usanii wenu hauna maana. Heri nicheze Jimmy Ngala mara mia.”
Kwa upande wake, Maria Cruize aliunga mkono marufuku hiyo kwa kusema:
“Pia kuimba nyimbo za watu marufukuu… kila mtu aimbe nyimbo zake.”
Wengine walienda mbali zaidi wakitaka marufuku hiyo ijumuishe nyimbo za wasanii wengine.
MV Tony Ke alisema:
“Hata nyimbo za Mbosso pia.”
Lakini si wote waliopinga. Baadhi ya mashabiki waliona Hosini Band kama kundi linaloleta utofauti na ubunifu mpya.
Chishengah Mungah aliandika:
“That’s why napenda Hosini.”
Wakati huo huo, Duncan Bongo alionesha masikitiko kuhusu matumizi ya kauli hiyo kwenye bendi nyengine akisema:
“Jana ule upande mwingine niliskia, hiyo ndio nyimbo… so sad.”
Ubunifu au Kuvuka Mipaka?
Mjadala huu umeibua swali kubwa katika tasnia ya muziki wa bango: Je, ubunifu unapaswa kuwa huru bila mipaka, au unapaswa kuzingatia maadili ya jamii?
Kwa msimamo wake, Bavyombo anaonekana kuchagua kulinda heshima ya sanaa na kuondoa lugha chafu ambayo imeanza kuingizwa kwenye nyimbo. Kwa wengine, hiyo ni hatua ya ujasiri; kwa wengine ni kuua burudani.
Kinachobaki wazi ni kuwa, Hosini Band sasa itaendelea bila kauli hiyo, na macho ya mashabiki yataelekezwa kuona kama mabadiliko haya yataleta muziki bora zaidi au yatapunguza mvuto wa bendi hiyo.
