Mwishoni mwa juma, tarehe 10 na 11 mwezi Januari 2025 Kenya ilijawa na hisia kinzani kuhusiana na ujio wa mwanamitandao kwa jina Ishow speed.
Mitandao ya kijamii ilisheheni hisia kinzani huku wakenya wa kizazi cha “milenia” Wakihusishwa na kuachwa nyuma katika kumtambua mzalishaji huyu wa maudhui maarufu kama Ishow speed.
Wengi wa kizazi hiki walionekana kuuliza maswali mengi mitandaoni wakiuliza kwa mshangao kuhusu Ishow speed.
Ni kitu, mtu au mahali?
Hebu nikupe tathmini kuhusiana na Ishow speed, wenzangu wazawa wa milenia huu sio mji, wala kifaa wala eneo, Ishow speed ni mzalishaji wa maudhui kwa kifupi mwana mitandao.
Darren Jason Watkins Jr ndilo jina lake halisi ila anajulikana kwa jina la msimbo Ishow speed.
Ishow speed alizaliwa Januari 21 mwaka 2005 kule Ohia, nchini Marekani.
Ni mtoto aliyelelewa na mzazi mmoja wa kike baada ya wazazi wake kutalikiana akiwa na umri mdogo akitokea kwenye familia ya watoto watatu.
Ishow speed ni mzalishaji wa maudhui kwa njia ya mtiririko wa moja kwa moja yani streamer kwenye mtandao wa YouTube.
Alianzisha akaunti yake ya YouTube mwaka 2016 akiwa na umri wa miaka 11.
Katika umri huu alianza kutumia mtandao kama ajira.
Ishow speed kufikia sasa anakadiriwa kuwa na utajiri wa Dola milioni 15 za Marekani ikiwa ni takriban bilioni 1.9 fedha za Kenya akiwa tu na umri wa miaka 21.
Mbali na kuwa mzalishaji maudhui ya mtiririko wa moja kwa moja, Ishow speed pia ni msanii wa muziki na mchekeshaji mwenye mihemko mikali ya makelele.
Ishow speed ni shabiki mkubwa wa nguli wa soka Cristiano Ronaldo.
Ishow speed alizuru Kenya na kupokelewa na umati mkubwa wa wakenya ambaye alitembelea maeneo mbalimbali.
Ziara yake imenufaisha vipi taifa la Kenya?
Bodi ya utalii nchini imesema ujio wa Ishow speed umeongeza idadi ya wanaofuatilia Kenya kwa upande wa utalii.
Na Hamisi Kombe
