Najua: Vybz Kartel Aigusa Afrika Mashariki kwa Neno Moja la Kiswahili

Najua: Vybz Kartel Aigusa Afrika Mashariki kwa Neno Moja la Kiswahili

Mwanamuziki maarufu wa Dancehall, Vybz Kartel, amesisimua mashabiki mtandaoni baada ya kujibu comment kwa lugha ya Kiswahili.

Msanii huyu kutoka Jamaica, anayejulikana pia kama World Boss, aliwashangaza wafuasi wake wa Afrika Mashariki kwa majibu hayo, ishara tosha ya upeo wa ushawishi wake duniani.

Tukio hilo lilitokea kwenye ukurasa wake wa Instagram, baada ya shabiki kuandika, ‘Wewe sasa ume zidi’. Kartel, anayejulikana kwa majibu yake ya papo kwa papo na ucheshi kwenye mitandao ya kijamii, alijibu kwa maneno mafupi: ‘Najua’.

Jibu hilo lilienea kwa kasi mtandaoni, huku mashabiki kutoka Kenya na Tanzania wakimiminika kwenye sehemu ya maoni.

Wengi walifurahia kuona Kartel akitumia Kiswahili, lugha inayozungumzwa sana Afrika Mashariki.

Kwa mashabiki wengi, jibu lake la neno moja lilithibitisha kwamba Kartel amekuwa akifuatilia kwa karibu mashabiki wake wa Afrika Mashariki, ambapo muziki wa dancehall una mashabiki wa dhati.

Katika wiki za hivi karibuni, msanii huyu mashuhuri amekuwa akitrend kutokana na vipande vya video vya burudani, akionekana akijibebea midundo na sauti maarufu.

Cha kuvutia ni kwamba baadhi ya sauti hizo zinazovuma zimetokea Kenya, jambo linaloongeza ukaribu wake na mashabiki wa Afrika Mashariki.

Mtindo wake huu wa kuburudisha umeibua mijadala kuhusu jinsi nyota wa kimataifa wanavyozidi kuunganishwa na mashabiki wa Kiafrika kwa njia za kipekee na zinazohusiana moja kwa moja na maisha yao.