Burudani Bila Malipo? Zuchu Aishtumu CAF

Burudani Bila Malipo? Zuchu Aishtumu CAF

Malkia wa Bongo Flava, Zuchu, ametuhumu hadharani Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kwa kushindwa kumlipa baada ya kutumbuiza katika fainali za Mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) 2024.

Kupitia mitandao yake ya kijamii, Zuchu ameonyesha wazi kutoridhishwa na CAF pamoja na mawakala wao, akilalamikia kutolipwa stahiki zake licha ya kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Malalamiko hayo ya msanii huyo yamewekwa wazi kupitia chapisho kwenye ukurasa wake wa Instagram lenye kichwa cha habari: “Malipo ya CHAN 2024 Bado Hayajatolewa kwa Onyesho Lililokamilika.”

Malalamiko hayo yanahusu ucheleweshaji wa malipo kufuatia onyesho alilolifanya tarehe 30 Agosti 2025 jijini Nairobi, Kenya.

Kupitia chapisho lake, Zuchu alieleza kuwa malipo hayo yalipaswa kulipwa mara moja baada ya onyesho, kulingana na makubaliano yaliyofikiwa na kampuni ya LEAP Creative Agency, waliokuwa wakala walioteuliwa na CAF.

“Natumai ujumbe huu unakufikia salama. Ninaandika kueleza hofu na kukatishwa tamaa kwangu kuhusu malipo ambayo hadi sasa sijapokea kufuatia onyesho langu la hivi karibuni jijini Nairobi, tarehe 30 Agosti 2025,” Zuchu alilalamika.

Timu ya usimamizi ya Zuchu imekuwa ikifanya mawasiliano ya mara kwa mara na wakala husika, lakini hadi sasa tatizo hilo halijapatiwa suluhisho.

Msanii huyo alieleza kuwa timu yake ilitumiwa vielelezo vya malipo ambavyo havikuweza kuthibitishwa, vilikuwa na mashaka, na kwa wazi kabisa havikuonyesha kuwa malipo hayo yalishawasilishwa. Hali hiyo ilimfanya kuamini kuwa kuna ucheleweshaji wa makusudi katika kutekeleza wajibu wa kifedha.

Zuchu alionyesha masikitiko, akisema licha ya yeye kutimiza kikamilifu sehemu yake ya makubaliano kwa kutoa onyesho la kiwango cha juu, bado hajalipwa. Aidha, alifichua kuwa alikataa mialiko mingine ya matamasha ili kutoa nafasi kwa tukio hilo la fainali za CHAN.

“Ni jambo la kusikitisha sana kuona kwamba kiwango kilekile cha weledi ambacho mimi nilikionyesha hakijarejeshwa upande wa utekelezaji wa wajibu wenu wa kifedha,” alisema Zuchu.

“Kama msanii, natarajia kutendewa kwa heshima na haki ambayo kila msanii wa kitaalamu anastahili. Ucheleweshaji huu siyo tu kwamba hauna haki, bali pia haukubaliki kabisa. Kama msanii, nililazimika kufuta matamasha mengine niliyokuwa nimepangiwa ili kutoa nafasi kwa tamasha hili la fainali. Sikutegemea kutendewa kwa njia isiyo ya haki namna hii,” aliongeza.

Zuchu, alikuwa miongoni mwa wasanii waliopamba tamasha la kufunga pazia la mashindano ya CHAN 2024, yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Moi, Kasarani, jijini Nairobi.

Zuchu alitumbuiza jukwaa moja na Eddy Kenzo kutoka Uganda pamoja na Savara kutoka Kenya — katika usiku wa burudani uliowakutanisha mastaa wakubwa wa muziki kutoka ukanda wa Afrika Mashariki.

Mashindano hayo yalikuwa ya kihistoria, kwani kwa mara ya kwanza yalifanyika kwa ushirikiano wa pamoja kati ya Kenya, Tanzania, na Uganda. Uamuzi wa kushirikiana katika uandaaji wa CHAN 2024 ulitafsiriwa kama ishara ya mshikamano na maono ya pamoja kwa mustakabali wa soka la ukanda huu.

Mchezo wa fainali uliwakutanisha mabingwa wa mara mbili Morocco, dhidi ya Madagascar waliokuwa wakicheza fainali yao ya kwanza kabisa katika historia ya mashindano haya.