Mojawapo ya sauti kubwa zaidi nyuma ya mafanikio ya muziki wa wasanii wengi Kenya, Producer lejendari J-Crack, amezungumza na Coco FM kuhusiana na posti ya Susumila aliyosherehekea miaka 18 tangu kutolewa kwa wimbo wa kihistoria – Siasa Duni.
Katika mahojiano hayo, J Crack hakuishia tu kupongeza kazi hiyo, bali alichambua kwa kina maana halisi ya kazi kama hiyo kwa kizazi cha sasa, huku akifichua changamoto kali alizokumbana nazo hivi karibuni.
“Siasa Duni” Ni Timeless – Na Sio Wimbo Wetu Tu
Kwa maneno yenye uzito mkubwa, J Crack alisema: “Siasa Duni ni wimbo timeless wenye impact sana. Ule wimbo hauna mipaka na hauna time. Ni wimbo mkubwa sana – classic. Sio wetu pekee yetu lakini pia kila nchi duniani. Huo ndio wimbo mkubwa sana ambao umebaki imara zaidi kati nyimbo zote za siasa.”
Kwa J Crack, Siasa Duni si kazi ya kawaida, bali ni kazi iliyopenya mipaka ya wakati na kijiografia, na inastahili kuheshimiwa kama nyimbo za kizazi kilichotangulia kilichotumia muziki kama silaha ya mabadiliko.
Katika ujumbe wa moja kwa moja kwa wanasiasa na viongozi, J Crack alitoa rai ya dhati: “Sio upatane na watu kidogo uamue kile unachotaka kufanya. Wanasiasa waingie nyanjani, wapate maoni ya wananchi na masaibu yao… Watuskize vilio vyetu.”
Akiwa amezuru nchi kadhaa, J Crack alisema amejionea jinsi wanasiasa wa mataifa mengine wanavyoshirikiana moja kwa moja na wananchi kuleta maendeleo – jambo ambalo, kwa mtazamo wake, bado ni changamoto Kenya.
Akizungumzia hali ya muziki kwa kizazi kipya, Producer huyo mkongwe alisema wazi kuwa vijana wengi wa sasa hawataki kusikiliza wazee wa game, na wanakimbilia staili za nje kabla ya kujifunza misingi:
“Unajua mara nyingine hawataki kutuskiza sisi ambao tumekaa sana… Wakiamini wanauwezo kwa sababu wanasikiliza kina Drake, sawa. Ila nasi tukitoa vitu vyetu – tutapiga hela. Mziki unabadilika ndio, lakini je, kile unachokiimba kinarelate na watu ambao unawaimbia?
Hii ni changamoto kwa wasanii chipukizi: kuunda kazi zenye maana, si tu za virality. Muziki unaobeba ujumbe wa jamii, kama Siasa Duni, haupitwi na wakati.”
Masaibu ya Studio
Mbali na mijadala ya muziki, J Crack alifunguka pia kuhusu tukio la kusikitisha – kuporwa vifaa vyake vya kazi, tukio ambalo liliathiri uendeshaji wa studio na miradi aliyokuwa akifanyia kazi: “Polisi walifika, wakaja kuangalia vile kulikuwa… Wakapiga picha na kuniacha ning’ang’ane ila sijafa moyo… vyombo sijavipata. Hakuna kilichoonekana mahali kinauzwa.”
Kwa juhudi binafsi, J Crack amesema ameanza kujikusanya tena sawa:
“Waliachia speaker ndogo na microphone. Nimenunua CPU, TV, sound card, na speaker… Tumeungaunga na tunasonga mbele.”
Miradi Iliyoathirika: Hasara Inayokaribia Milioni
Kulingana na Producer huyo, miradi kadhaa ya muziki iliharibiwa katika tukio hilo – ikiwemo EP iliyokuwa na nyimbo 9, na pia baadhi ya kazi za wasanii wengine kama Susumila: “EP ilikuwa na nyimbo 9… Project nyingine nilikuwa nimemaliza, niko nazo, lakini master zenyewe sina. Kuna project za Susumila pia. Media ikamnukuu vibaya… Lakini ukweli ndio huo.”
Kwa makadirio yake, hasara ya vifaa na kazi za muziki iliyopotea inakadiriwa kuwa:
“Hesabu za haraka upesi vi kwamba nimepoteza kati ya Ksh 250k na Kshs 300k ya vifaa vilivyoibwa. Ukichanganya na project zilizokuwa kwa mpango, inafika zaidi ya milioni.”
Producer huyo ametoa mwito wa wazi kwa kizazi kipya akisema; “Watuskize… Wako na vitu vya kujifunza kutoka kwetu.”