Cardi B Atangaza Ujauzito Kwenye Mahusiano yake Mapya na Stefon Diggs

Cardi B Atangaza Ujauzito Kwenye Mahusiano yake Mapya na Stefon Diggs

Rapa maarufu duniani, Cardi B, mwenye umri wa miaka 32, ametangaza kuwa anatarajia mtoto wake wa nne, na huyu atakuwa wa kwanza na mpenzi wake mpya, mchezaji wa NFL, Stefon Diggs.

Akitangaza habari hizo katika mahojiano na Gayle King kwenye kipindi cha CBS Mornings, Cardi B alithibitisha kuwa anatarajia kujifungua kabla ya kuanza ziara yake inayosubiriwa kwa hamu mwezi Februari mwakani.

“Natarajia mtoto na mpenzi wangu, Stefon Diggs,” alisema Cardi katika kipande cha mahojiano kilichorekodiwa awali. Nyota huyo aliyezaliwa Bronx, ambaye jina lake halisi ni Belcalis Almanzar, aliongeza kuwa anajisikia “mwenye furaha” na “amefurahishwa” na ujauzito huo.

“Nahisi niko katika nafasi nzuri. Najisikia mwenye nguvu sana, mwenye uwezo mkubwa kwamba ninafanya kazi yote hii huku nikibeba mimba,” alieleza.

Tangazo lake linakuja wakati anajiandaa kuachia albamu yake ya pili, Am I the Drama?, kesho tarehe 19 Septemba. Mradi huu—ambao ni wa kwanza tangu albamu yake ya mwaka 2018 iliyoshinda Grammy, Invasion of Privacy—unatarajiwa kuwa na ushirikiano mkubwa na wasanii wakubwa kama Janet Jackson, Selena Gomez, na Lizzo.

Cardi B alimsifia Stefon Diggs kwa namna anavyomfanya ajisikie salama, akisema:

“Ananifanya nijisikie salama, nina kujiamini, na mwenye nguvu. Wiki mbili zilizopita, nilikuwa karibu kupata mshtuko wa hofu kuhusu uzinduzi wa albamu, lakini alinisaidia kutulia. Kujisikia salama na kuwa na kujiamini kunakufanya uhisi unaweza kuuteka ulimwengu.”

Cardi B na Diggs walihusishwa kimapenzi kwa mara ya kwanza mwezi Oktoba mwaka jana. Walithibitisha uhusiano wao rasmi mwezi Mei walipohudhuria pamoja mechi kati ya Boston Celtics na New York Knicks katika ukumbi wa Madison Square Garden.

Stefon Diggs ni nani?

Stefon Diggs, mwenye umri wa miaka 31, ni mchezaji wa nafasi ya wide receiver katika ligi ya NFL, ambaye hivi karibuni amejiunga na timu ya New England Patriots baada ya kung’ara kwa misimu kadhaa akiwa na Buffalo Bills.

Diggs anajulikana kwa kasi yake, ustadi wa kukimbia njia za pasi (route-running), na uwezo wake wa kushika mipira migumu (game-changing catches). Amechaguliwa mara kadhaa kushiriki Pro Bowl na anachukuliwa kama mmoja wa wachezaji bora zaidi wa nafasi yake katika ligi hiyo.