Sports
Duplantis Awinda Taji la Tano Diamond League, Lyles na Tebogo Kukutana Zurich
Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya kuruka kwa mlingoti, Armand ‘Mondo’ Duplantis, analenga kushinda taji lake la tano mfululizo la Diamond League hii leo mjini Zurich, jiji la Uswizi linaloandaa fainali za mashindano hayo wiki mbili tu kabla ya mashindano ya dunia jijini Tokyo.
“Nalazimika kuzingatia kwa makini, siwezi kulegeza kamba,” alisema Mswidi huyo aliyezaliwa Marekani, ambaye amekuwa katika kiwango cha juu, akiweka rekodi yake ya dunia ya 13 ya mita 6.29 mjini Budapest mapema mwezi huu.
“Matumaini makubwa ni bora kuliko kutokuwa na matumaini. Ni changamoto nzuri, kwa kweli,” aliongeza akizungumzia matarajio ya mashabiki kuhusu hali ya sasa ya mashindano ya kuruka kwa mlingoti.
Lyles dhidi ya Tebogo;
Mabingwa 26 waliobakia wa Diamond League watajulikana katika ratiba ndefu kwenye Uwanja wa Letzigrund siku ya Alhamisi.
Watazamaji wataweza kushuhudia nyota wakubwa wa dunia akiwemo Noah Lyles na Letsile Tebogo, mabingwa wa Olimpiki katika mbio za 100m na 200m.
Wawili hao watakabiliana katika mbio za wanaume za 200m, ambapo Tebogo kutoka Botswana anawinda taji lake la kwanza kabisa la Diamond League, huku Mmarekani Lyles akitafuta kushinda taji hilo kwa mara ya sita, rekodi mpya.
“Kwa kuwa mbio za Weltklasse Zurich ndizo za mwisho kabla ya mashindano ya dunia, nataka kukimbia kwa kiwango cha juu kabisa,” alisema Lyles, ambaye alilazimika kuridhika na medali ya shaba katika Olimpiki za Paris kwenye mbio za 200m zilizoshindiwa na Tebogo.
Bingwa wa Olimpiki na Diamond League, Julien Alfred, pia atashiriki katika mbio za wanawake za 100m, huku nyota wa 800m Emmanuel Wanyonyi na bingwa wa kuruka viunzi vya 400m Femke Bol wakilenga kutetea mataji yao.
Wengi wa wanariadha wamefuzu kwa fainali za Diamond League kutokana na pointi walizokusanya kwenye mashindano 14 yaliyopita, huku wachache wakipata nafasi kupitia tiketi maalum za kimataifa au kitaifa.
Hata hivyo, Jakob Ingebrigtsen hatashiriki katika mbio za wanaume za 1,500m kwa angali anauguza jeraha la msuli wa paja.