Sports
Djokovic akutana na Alcaraz kwenye nusu fainali ya US Open, Sabalenka apenya bila kucheza
Mchezaji wa Tenisi Novak Djokovic amefuzu kwenye mechi ya nusu fainali ya US Open dhidi ya Carlos Alcaraz siku ya Jumanne huku bingwa mtetezi wa upande wa wanawake Aryna Sabalenka akitinga nusu fainali bila hata kunyanyua raketi yake.
Djokovic alizima matumaini ya Taylor Fritz ya kuwa Mmarekani wa kwanza kushinda taji la Grand Slam la wanaume tangu mwaka 2003 baada ya ushindi wa seti 6-3, 7-5, 3-6, 6-4 kwenye robo fainali iliyochezwa uwanjani Arthur Ashe Stadium.
Ushindi huo ulimpeleka Mserbia huyo mwenye umri wa miaka 38 ambaye anawinda taji la kihistoria la Grand Slam la 25 kwenye nusu fainali ya kusisimua dhidi ya Alcaraz, anayeshikilia nafasi ya pili duniani kutoka Uhispania, siku ya Ijumaa.
Djokovic alihitimisha ushindi wake pale Fritz, aliyeshika nafasi ya nne kwa ubora, alipofanya kosa la mara mbili la “double fault” kwenye “match point” katika mchezo wa 10 wa seti ya mwisho, na hakuficha furaha yake baada ya kuibuka mshindi.
“Katika mechi ya aina hii, pointi chache tu upande mmoja au mwingine ndizo huamua mshindi,” alisema. “Ilikuwa mechi ya karibu sana. Kwa kweli ingeweza kwenda kwa yeyote.”
Fritz aliachwa akijuta kushindwa kutumia fursa zilizojitokeza, baada ya kufanikisha ushindi wa pointi mbili pekee kati ya 13 katika pambano lililochukua saa tatu na dakika 24.
Mmarekani huyo alipoteza nafasi tano za “break point” katika seti ya kwanza ambazo zingemfanya aongoze 5-4, badala yake akamruhusu Djokovic kuponyoka na kuongoza kwa seti moja.
Baada ya kupambana na kufanikiwa kumsawazisha Djokovic kwa 5-5 katika seti ya pili, Fritz alivunjwa tena mara moja na kupoteza mwelekeo. Djokovic alishikilia na kuchukua uongozi wa seti mbili, na ingawa Fritz alirudi na kushinda seti ya tatu, Mserbia huyo mkongwe alikusanya nguvu upya na kumaliza kazi kwenye seti iliyofuata.
“Nilihisi nimebahatika sana kuokoa ‘break points’ muhimu katika seti ya pili,” Djokovic alisema. “Naamini kwa sehemu kubwa ya seti ya pili na ya tatu, alikuwa mchezaji bora zaidi.”
Djokovic atakutana na Alcaraz kwenye nusu fainali huku Mhispania huyo mwenye umri wa miaka 22 akiwa kwenye kiwango cha juu mno. Bingwa wa mara tano wa Grand Slam alihitaji saa moja na dakika 56 pekee kumshinda kwa urahisi Jiri Lehecka wa Jamhuri ya Czech, anayeshika nafasi ya 20, kwa seti 6-4, 6-2, 6-4.
Alcaraz hajapoteza seti yoyote kwenye safari yake ya kufuzu nusu fainali na mara nyingine tena alikuwa na udhibiti kamili dhidi ya Lehecka.
“Nilicheza mechi nzuri sana — karibu mechi kamilifu,” alisema Alcaraz, ambaye ameshinda mechi 35 kati ya 36 zilizopita tangu kuanza kwa Mashindano ya Italian Open mwezi Mei. “Inaonekana kama, sawa, zimebaki hatua mbili tu, tuone itakuwaje. Lakini naamini najihisi vizuri sana na nina njaa ya kuendelea kushinda.”
-
Sabalenka apita kwa ‘walkover’ –
Katika upande wa wanawake siku ya Jumanne, namba moja duniani na bingwa mtetezi Sabalenka alitinga nusu fainali baada ya mpinzani wake wa robo fainali kutoka Jamhuri ya Czech, Marketa Vondrousova, kujiondoa kutokana na majeraha ya goti.