Entertainment
Diddy Apatikana Bila Hatia Katika Mashtaka Mazito, Lakini Asalia Gerezani
Jopo la majaji 12 mjini New York limempata msanii maarufu wa muziki wa hip hop, Sean “Diddy” Combs, bila hatia katika mashtaka mazito yaliyomkabili, ambayo yangeweza kumpeleka kifungoni maisha.
Hata hivyo, Combs hataachiwa huru mara moja, baada ya jaji kukataa ombi lake la dhamana – na bado anakabiliwa na kifungo cha hadi miaka 20 jela kufuatia kutiwa hatiani kwa makosa mawili ya kusafirisha watu kwa ajili ya ukahaba.
Wataalamu kadhaa wa sheria wanasema huenda asitumikie kifungo hicho chote.
Jaji alitaja kukiri kwa upande wa utetezi kwamba Combs alijihusisha na ukatili wa majumbani katika mahusiano yake ya karibu kama sababu kuu ya kukataa ombi la dhamana.
Ingawa aliachiliwa huru kwenye mashtaka mazito zaidi, kesi hiyo ilijaa ushahidi uliotolewa na wapenzi wa zamani waliotoa maelezo ya kina kuhusu manyanyaso ya kimwili na ukatili wa majumbani.
Mawakili wa Combs walikubali kuwa alikuwa mkatili katika mahusiano yake, lakini walikanusha kuwa hilo linathibitisha kwamba alikuwa anaendesha mtandao wa kihalifu wa usafirishaji watu kwa ajili ya ngono.
Combs, ambaye amekuwa gerezani Brooklyn tangu Septemba mwaka jana, atasalia huko hadi tarehe ya kusikilizwa kwa hukumu yake tarehe 3 Oktoba.
Kesi hii imevutia umakini mkubwa. Diddy ni mmoja wa wasanii mashuhuri wa hip hop nchini Marekani, na hakuwa ameonesha dalili zozote za kustaafu kabla ya kukamatwa kwake. Kwa sasa, mustakabali wake wa karibu – pamoja na urithi wake katika muziki wa rap – bado haujajulikana.