Entertainment
Creative Economy Forum 2025: Ruby Kache Uso kwa Uso na Bien
Ruby Kache na Bien wakutana Nairobi kwenye Jukwaa la Uchumi wa Ubunifu! 🌟
Jiji la Nairobi liling’aa zaidi wiki hii baada ya kuandaa Jukwaa la Uchumi wa Ubunifu — tukio la kipekee lililowakutanisha wabunifu, wanamuziki, na wadau wa sanaa kutoka Kenya na Marekani. Mbali na mijadala ya sera na mipango ya maendeleo, tukio hili lilikutanisha watu mashuhuri.
Mrembo wa redio, Ruby Kache, alikutana na nyota wa muziki, Bien aliyekuwa kwenye kundi la maarufu Sauti Sol!
Kwa wanaosikiliza redio, jina la Ruby Kache si geni. Ni mtangazaji machachari wa kipindi cha “The Wave” kupitia Coco FM, kinachoenda hewani kila Jumamosi kuanzia saa 4 asubuhi hadi saa 7 mchana. Kipindi chake kinajulikana kwa kuangazia maisha ya vijana, muziki wa kisasa, mitindo na mazungumzo yenye msisimko.
Katika kongamano hili, Ruby alihudhuria kama mshiriki, lakini kama ilivyo kawaida yake — aliiba spotlight bila kusema neno jukwaani. Uvaaji wake, tabasamu lake na muingiliano wake na wadau wengine ulitosha kuonyesha uwepo wake wa nguvu.
Moja ya highlights kubwa za siku hii ilikuwa ni wakati Ruby Kache alipokutana na Bien. Ruby alirekodi kipande kifupi na kukipakia kwenye ukurasa wake wa Facebook, huku mashabiki wakishangilia. Bien, nguli wa mziki anayeshikilia tuzo ya muimbaji bora Afrika Mashariki, alikuwa mgeni maarufu katika tukio hilo.
Baadhi ya waunda maudhui maarufu kutoka Pwani waliopamba hafla hiyo ni pamoja na Presenter Kai, Beka Ruga, Mwagwaya Ndani, na Princess Fynick, waliokuja kwa mitoko ya kisasa. Kwa upande wa muziki, Reagan Dandy alikuwa miongoni mwa wanamuziki wachache kutoka Pwani waliobahatika kuhudhuria tukio hilo la hadhi ya kimataifa.
Jukwaa la Uchumi wa Ubunifu limeibuka kama jukwaa muhimu kwa kuvunja mipaka kati ya sanaa, biashara na teknolojia. Kupitia mikutano kama hii, wasanii, waunda maudhui na wadau wa sekta ya ubunifu wanapata nafasi ya kuunganishwa na fursa za kimataifa, kujifunza kuhusu ulinzi wa kazi zao, na kuelewa jinsi ya kujitegemea kiuchumi kupitia vipaji vyao. Kwa kizazi kinachotegemea mitandao na ubunifu kama njia ya kujieleza, majukwaa haya yanakuwa daraja kati ya ndoto na mafanikio halisi.
Kwa washiriki kutoka Pwani na sehemu nyingine za Kenya, kongamano hili halikuwa tu mahali pa kuonekana, bali pa kujifunza, kuunganishwa na kuchochewa kufikiria ubunifu kama ajira na biashara. Uwepo wa majina maarufu kama Ruby Kache, Bien, na waunda maudhui wengine wakubwa ulitoa motisha kwa vijana, huku ikithibitisha kuwa sanaa inaweza kuwa nguvu ya kiuchumi na chombo cha mabadiliko chanya katika jamii.