Entertainment

Chris Brown Akanusha Shtaka la Kumshambulia Producer kwa Chupa

Published

on

Msanii nyota wa Marekani, Chris Brown, amekana mashtaka mawili mahakamani yanayohusiana na madai ya shambulio kwa kutumia chupa katika kilabu cha usiku jijini London miaka miwili iliyopita.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 36 anatuhumiwa kumsababishia mtayarishaji wa muziki majeraha ya mwili katika tukio ambalo waendesha mashtaka wamelieleza kuwa “halikuwa na uchochezi wowote”.

Pia anakabiliwa na shtaka la kumiliki silaha hatari — ambayo ni chupa ya kileo.

Mashtaka haya mawili yaliongezwa mwezi uliopita kwenye shtaka la awali, kubwa zaidi, la kujaribu kumsababishia mtu majeraha mabaya ya mwili (GBH), ambalo tayari Bwana Brown alilishatupilia mbali kwa kujitetea kuwa si kweli.

Chris Brown anatarajiwa kufikishwa mahakamani kwa kesi hiyo mwezi Oktoba mwaka 2026.

Waendesha mashtaka wamesema kuwa mhanga wa tukio hilo, Abraham Diaw, alikuwa amesimama kwenye baa ya kilabu cha usiku kilichopo eneo la Soho mnamo tarehe 19 Februari 2023, wakati Chris Brown alimpiga kwa chupa mara kadhaa.

Mwimbaji huyo alikamatwa mwezi Mei katika hoteli ya nyota tano iliyopo Salford, Greater Manchester, baada ya kurejea Uingereza kwa ajili ya maandalizi ya ziara yake ya muziki barani Ulaya.

Alizuiliwa korokoroni kwa takriban wiki moja kabla ya kuachiliwa kwa dhamana baada ya kukubali kulipa ada ya dhamana ya pauni milioni tano (£5m) kwa mahakama.

Ada ya dhamana ni kiasi cha fedha kinachowekwa kama dhamana ya kifedha kuhakikisha mtuhumiwa atarudi mahakamani kwa kesi yake. Brown anaweza kupoteza fedha hizo endapo atakiuka masharti ya dhamana, ambayo yaliendelezwa katika kikao cha mahakama siku ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa masharti hayo, Chris Brown anatakiwa kuishi katika anwani iliyopo Uingereza akisubiri kesi hiyo, na aliamriwa kukabidhi pasipoti yake kwa polisi.

Hata hivyo, ameruhusiwa kuendelea na ratiba ya ziara yake ya kimataifa ya Breezy Bowl XX kwa masharti kwamba atakabidhi pasipoti kila anapomaliza safari, na kuirudishiwa anapohitaji kusafiri kwa ajili ya maonesho.

Katika wiki za hivi karibuni, Brown amekuwa akitumbuiza kwenye viwanja na kumbi mbalimbali za burudani kote Uingereza na Ulaya, na kumaliza burudani mjini Paris mwishoni mwa wiki iliyopita. Sehemu ya ziara hiyo inayofanyika Marekani Kaskazini inatarajiwa kuanza baadaye mwezi huu na kufikia tamati tarehe 18 Oktoba.

Kikao kingine cha mahakama kimepangwa kufanyika tarehe 24 Oktoba.

Chris Brown ni miongoni mwa wanamuziki wakubwa zaidi wa R&B nchini Marekani, akiwa mshindi wa tuzo mbili za Grammy na nyimbo 19 zilizofika katika nafasi 10 za juu kwenye chati za Uingereza, zikiwemo Turn Up The Music, Freaky Friday, With You na Don’t Wake Me Up.

Mshitakiwa mwenza, Omololu Akinlolu, raia wa Marekani mwenye umri wa miaka 39 anayefahamika kisanii kama HoodyBaby, naye pia alikana shtaka la kumsababishia mtu majeraha ya mwili. Awali, alikana pia shtaka la kujaribu kusababisha majeraha mabaya ya mwili.

Chanzo: BBC

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version