Serikali yachukua hatua za haraka kupunguza bei za mafuta

Serikali yachukua hatua za haraka kupunguza bei za mafuta

Mamlaka ya kudhibiti bei ya mafuta nchini EPRA imetangaza kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya Petroli, Dizeli na Taa humu nchini.

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Mamlaka hiyo Mhandisi Joseph Oketch katika taarifa aliyoitoa, ametangaza kupunguzwa kwa bei ya mafuta ya petroli kwa shilngi 9.37, mafuta ya Dizeli kwa shilingi 10.21 huku bei ya mafuta ya Taa ikisalia kama kawaida.

Oketch amesema hatua hiyo ni baada ya Hazina ya kitaifa kupunguza ushuru wa mafuta kwa asilimia 8 kutoka asilimia 13 ili kuchangia kupungua kwa gharama ya ununuzi wa mafuta baada serikali kutenga shilingi bilioni 6.5 za ruzuka ya mafuta.

Hatua hii imejiri mda mchache tu baada ya Mamlaka hiyo awali kutangaza bei ya mafuta ya Petroli kupanda kwa shilingi 28 kwa lita na mafuta ya Dizeli yakipanda kwa shilingi 40 kwa lita, hatua iliyosababisha viongozi wa upinzani kutishia kuitisha maandamano ya kitaifa kushinikiza kupunguzwa kwa bei hizo za mafuta nchini.

Hata hivyo katika taarifa ya Mamlaka ya EPRA, ilisema mafuta ya Petroli sasa yatauzwa kwa shilingi 197.60 kwa lita, huku mafuta ya Dizeli yakiungwa kwa shilingi 196.63 kwa lita na mafuta ya Taa yakisalia shilingi 152.78 kwa lita, katika jiji la Nairobi.

Mjini Mombasa, bei ya mafuta ya Petroli sasa itauzwa kwa shilingi 194.32, mafuta ya Dizeli yakiuzwa kwa shilingi 193.35 huku mafuta ya Taa yakiuzwa kwa shilingi 149.49 kwa lita na mjini Kilifi bei hiyo ya mafuta ikipungua na mafuta ya Petroli sasa yatauzwa kwa shilingi 195.18, mafuta ya Dizeli yakiuzwa kwa shilingi 194.22 huku mafuta ya Taa yakiuzwa kwa shilingi 150.36 kwa lita.

Hata hivyo Mamlaka hiyo imesema tangazo hilo limezingatia notisi ya kisheria nambari 70 na kwamba bei hiyo mpya ya mafuta inaanza kutekelezwa mara moja na itadumu kwa kipindi cha mwezi mmoja hadi tarehe 14 mwezi Mei mwaka huu.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi