Kituo cha kitaifa cha kukabiliana na ugaidi yaani National Counter Terrorism Centre (NCTC) kimeanzisha mpango wa kutoa hamasa za kuwaepusha wananchi na masuala ya ugaidi hasa maeneo ya Shakahola katika eneo bunge la Magarini kaunti ya Kilifi.
Akizungumza katika eneo hilo, Afisa mkuu wa kituo hicho Grace Kaparo aliwataka wazazi kufuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao kama njia mojawapo ya kuzuia michipuko ya makundi ya ugaidi.
Kaparo alidokeza kwamba mpango huo unalenga kupunguza visa vya uhalifu miongoni mwa vijana sambamba na kuwajengea mustakabali bora wa maisha yao.
Hamasa hiyo inajiri baada ya kushughudiwa maafa ya watu zaidi ya 400 katika msitu wa Shakahola kutokana na mafunzo ya itikadi kali huku mshukiwa mkuu wa mauaji hayo akiwa katika mikono ya maafisa wa polisi.
“Tumekuja Shakahola kuelimisha jamii kuepusha makundi ya kigaidi na jinsi ya kutambua watu walio na itikadi kali ili kuepusha watu kuangamia kama hapa Shakahola watu wangekuwa na ufahamu wangeepuka maafa”, alisema Grace.
Kwa upande wake Naibu Kamishna eneo Malindi kaunti ya Kilifi Harrison Matevwa aliwataka maafisa wa utawala eneo hilo kuendeleza hamasa za mara kwa mara kwa wakaazi wa maeneo yao ili kutathmini changamoto zinazowakumba na kuzitatua mara moja.
“Naiambia kamati ya usalama eneo hili kutembea na kufanya baraza za usalama kuweza kuskia ile wananchi wanapitia kwa sababu wengi wanakosa usaidizi ndio watu wahalifu wakija wanaweza kuwapotosha”alisema Harrison.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
