Mahakama ya Kilifi imewahukumu kifungo cha mwaka mmoja gerezani baba na mwanawe wanaohusishwa na kesi ya tuhma za kupotea kwa sehemu nyeti.
Wawili hao Benson Ngala Daniel na Ruphus Chai walishtakiwa na kesi ya kumpiga na kumjeruhi vibaya mama mmoja kwa jina Asha Samini waliyedai kuwa alikuwa amewaibia sehemu nyeti baada ya kuwasalimia
Hukumu hiyo imetolewa baada ya upande wa mashtaka ukiongozwa na Nancy Njeru kuiomba Mahakama itilie maanani kesi hiyo, akisema kuwa uvumi unaoendelea Kilifi na Pwani kwa jumla kwamba watu kupotezewa nyeti umesababisha vifo na wengine kuachwa na majeraha mabaya huku wakiibiwa mali zao.
Akitoa hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike amesema kuwa kifungo hicho kitakuwa funzo kwa watu wote wanaopiga watu kwa kuwatuhmu uchawi wa kuiba sehemu nyeti.
Awali upande wa mashtaka ulielezea mahakama kwamba mnamo tarehe 5 mwezi huu wa Julai, eneo la Mdangarani eneo la Kauma kaunti ya Kilifi, Benson na Ruphus walimpiga vibaya mlalamishi hali iliyomsababishia majeraha mabaya na ya kudumu na sasa anaendelea na matibabu katika hospitali ya rufaa Kilifi.
Aidha Mahakama imeagiza mlalamishi kuendelea na matibabu na kupata ushauri nasaha kupitia ofisi ya jamii.
Wahukumiwa wamepewa siku 14 za kukata rufaa.
Taarifa ya Teclar Yeri
