Mahakama ya Malindi imewaamuru wakurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Direct Line kufika Mahakamani binafsi kwa ajili ya kuhojiwa.
Hii ni baada ya kampuni hiyo kushindwa kutekeleza amri ya Mahakama ya kulipa fidia ya shilingi milioni 2.26 kwa mwanamke aliyejeruhiwa vibaya katika ajali ya barabarani iliyokea Oktoba 6, mwaka 2016.
Kampuni hiyo, inayohusishwa na familia ya mfanyabiashara mashuhuri nchini ilishindwa kumlipa Hellen Waiyaki kiasi cha shilingi 2,259,825 kama ilivyoamriwa na Mahakama.
Waiyaki aliwasilisha kesi Mahakamani baada ya kampuni hiyo kukosa kutekeleza wajibu wake wa kulipa kiwango hicho cha pesa licha ya kuagizwa na Mahakama kufuatia ajali hiyo iliyohusisha basi la Tahir Sheikh Said Transporters Limited, maarufu kama TSS Bus Company, yenye nambari ya usajili KBZ 475S.
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mwandamizi wa Mahakama ya Malindi, Joy Wesonga, alisema ni lazima wakurugenzi hao wafike Mahakamani binafsi na kujieleza, akisema kampuni hiyo imekuwa ikiwazuia wananchi kufikia ofisi zao.
“Wakurugenzi hao watahitajika kufika mahakamani wakiwa na kuwasilisha vitabu vya hesabu vilivyokaguliwa vya kampuni, taarifa za benki pamoja na sajili ya mali za kampuni kwa kipindi cha miaka miwili ya mwisho ya kifedha ili Mahakama iweze kubaini uwezo wa kifedha wa kampuni hiyo na hali ya shughuli zake za kibiashara nchini Kenya.” alisema Hakimu Wesonga.
Katika hati kiapo kilichowasilishwa mahakamani kupitia wakili wake George Wakahiu, Hellen Waiyaki alisema alikuwa abiria ndani ya gari hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa kwa uzembe kabla ya kupinduka na kusababisha ajali iliyomwacha na majeraha mabaya mwilini.
Kesi hiyo itaendeleza mnamo Julia 31 mwaka huu.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
