Mamlaka ya AFA yahimiza upanzi wa mkorosho

Mamlaka ya AFA yahimiza upanzi wa mkorosho

Mamlaka ya Kilimo na Chakula nchini AFA, imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha taifa linaboresha mazao yake na kuchangia uzalishaji wa chakula nchini.

Hatua hii imechangia zaidi na mikakati endelevu ya kuwawezesha wakulima kufahamu mipango endelevu ya uimarishaji wa Kilimo cha sasa na kwa kuzingatia utumiaji wa mifumo bora ya kilimo.

Mamlaka hiyo ambapo inaendeleza kampeni ya kuhamisha wakulima kuhusu umuhimu wa kilimo cha Korosho imesisitiza haja ya ujumuishaji wa wakulima, wawekezaji na wadau mbalimbali ili kupiga jeki sekta ya Kilimo huku ikiahidi kuendeleza hamasa kwa jamii za kaunti za Pwani kuhusu kilimo cha korosho na utafutaji wa soko huru.

Katika Kongamano la kitaifa lililoandaliwa katika kaunti ya Kwale, Mamlaka hiyo iliwapa wakulima kutoka kaunti sita za Pwani miche ya mikorosho elfu mia moja katika juhudi za kukuza kilimo cha zao hilo nchini.

Katibu katika Idara ya Kilimo nchini Paul Kiprono, alisema mpango huo unalenga kuwawezesha wakulima kuongeza uzalishaji wa korosho na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Kiprono alitoa wito kwa serikali za kaunti pamoja na wadau wa sekta ya kilimo kushirikiana kwa karibu ili kuboresha kilimo cha korosho.

“Kenya ilikuwa ikiongoza katika zao la mkorosho katika miaka ya 1990 lakini kutokana na changamoto za kibiashara zao hilo lilishuka katika masoko ya kimataifa kutokana na ukosefu wa kuwekezaji kwa wakulima lakini sasa tumeanza kupiga hatua kwani tunazalisha zaidi ya tan elfu 9 za korosho”, alisema Rono.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa AFA, Cornelly Serem, alisema mamlaka hiyo imejizatiti kuboresha kilimo cha korosho kupitia utoaji wa miche bora na mafunzo kwa wakulima ili kuongeza tija.

Taarifa ya Mwanahabari wetu