Mgombea wa kiti cha ugavana wa kaunti ya Kilifi Aisha Jumwa amekihama rasmi chama cha UDA, akisema atatangaza baadaye mwelekeo atakaochukua wa kisiasa.
Jumwa alitoa tangazo hilo katika kikao na Wanahabari kilichofanyika katika makaazi yake, eneo la Kakuyuni huko Malindi kaunti ya Kilifi leo siku ya Alhamis.
Hatua ya Jumwa ilijiri baada ya kuwepo na tetesi kwamba alikuwa na mipango ya kuhama chama hicho kutokana na sintofahamu za kisiasa ndani ya chama cha UDA kuhusu msimamo wake wa kisiasa wa kuwania nafasi ya ugavana wa Kilifi.
Jumwa alilalamika kwamba alikuwa akinyanyaswa na baadhi ya viongozi hata kutimuliwa katika Ikulu ya rais licha ya kupambana katika kampeni za rais Ruto mwaka wa 2022, akionekana kumlaumu rais Ruto kwa kutomjali tena hata baada ya kusimama na yeye kisiasa.
Kiongozi huyo alikashfu vikali kutengwa katika mikutano ya UDA licha ya kuwa mwandani wa rais Ruto na pamoja na kufanyikisha miradi ya serikali mashinani, akisema tangu atangaze mchakato wa kuwania kiti cha ugavana wa Kilifi mwaka wa 2027, amekuwa akipitia masaibu mengi.
Hii sio mara ya kwanza kwa Jumwa kukihama Chama cha UDA na kurejea kwenye chama hicho, lakini hatua aliyoichukua sasa itabadili masimamo wa kisiasa kaunti ya Kilifi.
Itakumbukwa kwamba Jumwa amekuwa mwandani wa karibu wa rais William Ruto, lakini hatua aliyoichukua huenda ikabadili msimamo wa kisiasa kaunti ya Kilifi na Pwani kwa jumla.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
