News

Bitok: Serikali kusambaza fedha za shule wiki hii

Published

on

Serikali imetangaza kwamba Fedha za usimamizi wa shughuli za masomo katika shule za umma kote nchini zitasambazwa kabla ya wiki hii kukamilika ili kuwawezesha wanafunzi kuendelea na masomo yao.

Katibu katika Wizara ya Elimu nchini Julius Bitok alisema zaidi ya shule elfu 45 za umma kote nchini zitapokea mgao wa fedha ili kufanikisha shughuli za masomo, akisisitiza kwamba hatua hiyo itadhibiti changamoto za elimu.

Akizungumza na Wanahabari jijini Nairobi, Bitok alisema Wizara ya Elimu nchini ilifanya mazungumzo na Maafisa wa Hazina kuu ya fedha ikiwemo Waziri wa Fedha nchini John Mbadi na kuafikiana kusambazwa kwa shilingi bilioni 23.

“Tumehusisha hazina kuu ya kitaifa ya fedha na pia tumefanya mazungumzo maafisa wa hazina hiyo wakiongozwa na Waziri mwenyewe na tunataka kuwahakikisha wakenya kwamba tumeweka mikakati mwafaka na fedha za usimamizi wa shughuli za masomo zitasambazwa kwa shule elfu 45 kote nchini kabla ya kukamilika kwa wiki hii”, alisema Bitok.

Wakati huo huo, Bitok aliwarai walimu wakuu kote nchini kuhakikisha wanakumbatia kikamilifu mfumo mpya wa elimu nchini CBC, akisema tayari serikali imejitolea kuhakikisha inafanikisha mchakato mzima wa elimu nchini.

Taarifa ya Mwahoka Mtsumi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version