News
Mchakato wa kuwapiga msasa Makamishena waanza Bungeni
Bunge la kitaifa limeanza kuwapiga msasa makamishena wateule 7 wa tume ya Uchaguzi na mipaka, IEBC katika majengo ya Bunge.
Shughuli hiyo imeanza leo Jumamosi Mei 31 2025, kufuatia maagizo ya Mahakama kuu kuondoa marufuku ya awali iliyositisha zoezi hilo.
Hata hivyo wiki iliyopita Jaji wa Mahakama hiyo Lawrence Mugambi aliliagiza bunge la kitaifa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba wa kuwapiga msasa makamishena hao pamoja na mwenyekiti wake, ingawa ilizuia kuapishwa au kuchapishwa katika gazeti rasmi la serikali, majina ya Makamishna wapya wa tume hiyo, hadi mchakato huo utakapokamilika .
“ Bunge sasa linaweza kuendelea na zoezi la kuwapiga msasa makamishena hao 7 kufuatia uamuzi huu wa leo Mei 29 alisema Jaji mkuu Lawrence Mugambi ”
Uamuzi huu ulitolewa siku chache tu baada ya mahakama hiyo kusitisha zoezi hilo la kuwapiga msasa makamishena hao hadi pale kesi iliyokuwa imewasilishwa kotini na walalamishi wawili, Boniface Mwangi na Kelvin Roy Omondi, waliopinga uteuzi wa makamishena hao.
Makamishena hao wanaopigwa msasa ni Erastus Edung Ethekon mwenyekiti mteule,na makamishena Anne Nderitu, Moses Mukwana, Mary Karen Sorobit, Hassan Noor, Francis Odhiambo, na Fahima Abdalla,
Hii si mara ya kwanza zoezi la kuwatafuta makamishena wa IEBC kupatwa na pigo baada ya zoezi la kuwahoji watu waliopasa kuteuliwa katika nyadhifa hizo, pia kukumbwa vikwazo kufuatia kesi iliyowasilishwa mahakamani kupinga utaratibu uliodaiwa kuenda kinyume na ripoti ya NADCO ya kushirikisha maoni ya wananchi .