News

Wanaosajiliwa Kwenye Mpango wa Kazi “Majuu” Waonywa.

Published

on

Waziri wa Leba nchini Dakta Alfred Mutua amewaonya vijana waliopata nafasi za ajira ughaibuni dhidi ya kujihusisha na visa vya utovu wa nidhamu.

Akizungumza wakati wa zoezi la kusajili vijana kwenye mpango wa ajira za nje nchi maarufu Kazi “Majuu” katika kaunti ya Kwale, Waziri Mutua alitaja hatua hiyo kwamba huenda ikachangia kandarasi zao kufutiliwa mbali sawa na kukabiliwa kisheria.

Mutua alidokeza kwamba kuna baadhi ya vijana ambao tayari wamerejeshwa nchini kufuatia visa vya utovu wa nidhamu

“Unaskia unawashwa unataka kuandamana, unataka kuwa mwanaharakati, unataka kuchochea ingia ndege uje hapa wikendi moja uandamane kila mahali hiyo kitu ikutoke urejee kazini, kwa sababu ukienda kufanya huko maandamano unaharibia wakenya wengine, kuna watu waliandamana huko nchi tofauti tofauti, wakenya kumi na tano wengi wakasimamishwa, wakaregeshwa nyumbani, unaandamana kwa nchi nyengine wanauliza mbona mkenya anaandamana na mganda haandamani, mbona mtanzania haandamani”, alisema waziri Mutua.

Akizungumzia suala la utumizi wa dawa za kulevya, Waziri Mutua amewataka vijana hao kukomesha uraibu huo kwani  hakuna taifa linaloshabikia matumizi ya dawa za kulevya.

“Hapa utafanyia ukaguzi wa kiafya kama umekuwa ukivuta bangi, madawa ya kulevya utaanguka, hata ukikataa kupatikana hapa ukifika ng’ambo  utapatikana, kwa hivyo kama unataka kwenda ng’ambo achana na bangi bwana”,aliongeza waziri Mutua.

Zoezi hilo lililenga vijana 800 kaunti ya Kwale na 3,500 eneo la pwani kwa ujumla.

Taarifa ya Joseph Jira

 

 

 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version