Entertainment
Sikutaka Pesa, Nilitaka Furaha – Bango Likaleta Vyote, Manu Bayaz
Afisa wa polisi ambaye pia ni muimbaji wa muziki wa Bango, Emmanuel Yaa Baya anayejulikana zaidi kwa jina la kisanii Manu Bayaz, amefichua kilichomsukuma kuingia kwenye muziki wa Bango.
Akihojiwa na Coco FM katika kipindi cha Coco Asubuhi, Bayaz alisema kwamba hajaanza muziki kwa ajili ya kutafuta pesa, bali alitaka kujifurahisha tu. Hata hivyo, nyimbo zake zilianza kuvutia watu wengi na kumpatia umaarufu mkubwa miongoni mwa mashabiki wa muziki wa Bango wengine wakiitisha huduma zake kwenye sherehe zao.
“Hapo awali haikuwa kwa ajili ya pesa. Nilianza kwa kujifurahisha, lakini watu wakaanza kupenda nyimbo zangu,” alisema Bayaz.
Kutokana na mafanikio hayo, Bayaz aliamua kubadili mtazamo na kuanza kuwekeza zaidi kibiashara kwenye muziki huo.
Akiendelea kuelezea safari yake ya muziki, alitaja changamoto kubwa aliyokumbana nayo kuwa ni kudhibiti kundi la wanamuziki, akisisitiza ugumu wa kuwaunganisha watu wenye malezi na mitazamo tofauti katika kundi moja.
“Kwenye bendi, kila mtu ametoka mazingira tofauti, amekuzwa kivyake. Kuwaunganisha watu kama kumi si jambo rahisi, lakini tunajitahidi,” alisema.
Bayaz analikumbuka kwa furaha tukio la malipo yake ya kwanza katika muziki wa Bango.
“Malipo yangu ya kwanza ndiyo experience nayoikumbuka maisha yangu ya mziki. Nililipwa shilingi elfu hamsini za Kenya (KSh 50,000), Mtu wa kwanza kumtaarifu habari hii ni babangu,” alisimulia.
Alieleza pia kuwa mapenzi yake ya muda mrefu kwa muziki wa Rhumba ndiyo yaliyomsukuma kuimba Bango, akieleza kuwa Bango ni aina ya Rhumba yenye ladha ya Pwani.
“Mimi napenda sana Rhumba. Nilivyoanza kuimba nikaona niende kwenye hiyo njia. Bango ni Rhumba tu, ila lina ladha ya Kipwani.”
Bayaz alianza kuimba akiwa na Sumilani Band na baadaye Ministers Band. Hata hivyo, aliachana na Sumilani baada ya kutofautiana kuhusu jina jipya alilopendekeza kwa bendi hiyo.
Bayaz pia alieleza kuwa alinunua vyombo vyake vya muziki kutoka China ili kuimarisha safari yake ya muziki, huku akiendelea kufanya kazi na bendi ya Sumilani kabla ya kuondoka.