News
Kesi dhidi ya Mackenzie na washukiwa wenzake 38 inaendelea Mahakamani
Kesi dhidi ya mhubiri tata Paul Mackenzie na washukiwa wenzake 38 kuhusu ukatili na ukiukaji wa haki za watoto inaendelea kusikizwa katika mahakama ya watoto ya Tononoka kaunti ya Mombasa mbele ya hakimu mkuu Nelly Chepchirchir, mashahidi 3 wakishuhudia.
Shahidi wa 47 ambaye ni mtaalamu wa afya ya akili ya watoto kutoka kituo cha watoto cha Malindi kaunti ya Kilifi, ameeleza mahakama namna mvulana mmoja miongoni mwa watoto 8 waliookolewa kutoka kwenye msitu wa Shakahola alivyokuwa na msongo wa mawazo kutokana yaliyokumba msituni humo.
Amesema mtoto huyo ambaye alisimulia mateso ya kimwili ambapo alikuwa akipigwa kwa kukiuka sheria za Mackenzie na kuishi kwa mateso, hali ambayo ilimsukuma kukimbilia kituo cha biashara kutafuta msaada.
Mtaalamu huyo pia amesema baada ya tathmini ya kitaalamu, alipendekeza mazingira salama ya malezi ya mtoto huyo kwasababu alikuwa na hofu ya kurudishwa Shakahola.
Amesema pia licha ya watoto ambao ni Manusura kurudi katika hali yao ya kawaida kuna haja ya kuendelea kuwapa usaidizi wa kisaikolojia hasa kwa kuwa walikuwa na wasiwasi kuhusu walipo jamaa zao.