News
Wavuvi wataka KPA kumwaga tope eneo mbadala baharini
Wavuvi eneo bunge la Likoni, kaunti ya Mombasa, wameitaka halmashauri ya bandari nchini (KPA) kusitisha mara moja shughuli za kumwaga tope maeneo ya bahari wanakofanyia shughuli zao za uvuvi.
Wavuvi hao walisema tope hizo zimeathiri mazingira ya bahari na kuhatarisha maisha ya viumbe hai majini, hasa samaki ambao ni tegemeo lao kuu la kipato.
Wakizungumza wakati wa kikao cha hadhara cha kukusanya maoni ya wananchi kuhusu uandaaji wa mpango wa maendeleo ya kaunti wa mwaka wa fedha 2026/2027 wavuvi hao walieleza kuwa tope hizo zinatokana na upanuzi wa kina cha bandari, na kumwaga tope baharini kunasababisha uchafuzi wa maji na kuharibu mazalia ya samaki.
Wakiongozwa na Shaban Mohammed, waliitaka KPA kushirikiana na jamii za wavuvi kabla ya kutekeleza miradi yoyote inayohusisha maeneo ya bahari, na kutumia mbinu mbadala za utupaji wa tope zinazolinda mazingira na maisha ya wakazi.
“Wale watu wanaokuja kuchimba kula bandarini wanamwaga tope kwenye mazingira ya samakai ambako ndio maeneo tunavua samaki, hatujui ni eneo walipewa na wanaochimba kule au ni wao wenyewe wanafanya hivyo kwa sababu hawafiki mahali stahiki ya kumwaga zile taka”,alisema Mohammed
Aidha, gavana wa Mombasa, Abdulswamad Sharif Nassir, aliahidi kufuatilia suala hilo na taasisi husika ili kuhakikisha linaangaziwa na kutatuliwa kwa haraka.
Taarifa ya Mwanahabari.