Sports
Wanyonyi, Cherotich na Chepchirchir Washinda Fainali Diamond League Zurich, Kenya Yaandika Historia
Bingwa mtetezi wa Olimpiki katika mbio za mita 800, Emmanuel Wanyonyi, aliibuka mshindi wa taji la Diamond League baada ya kumshinda Max Burgin wa Uingereza katika fainali ya mbio hizo jijini Zurich, jana usiku.
Wanyonyi, ambaye anasubiri Kipute cha Dunia mjini Tokyo Japan ndani ya wiki mbili zijazo, alilazimika kutumia kasi ya mwisho ili kuzuia shambulizi la kasi la Mwingereza huyo katika hatua ya kumalizia. Akishinda kwa muda bora wa 1:42.37, huku Burgin akimaliza kwa muda wa 1:42.42.
Bingwa mtetezi wa Diamond League, Marco Arop wa Canada, alimaliza wa tatu kwa muda wa 1:42.57.
Ushindi wa Wanyonyi ukiashiria usiku wa kihistoria kwa Kenya, ambapo timu hiyo ilitwaa jumla ya medali tatu za Diamond League na medali ya fedha.
Mkenya mwingine Faith Cherotich, bingwa wa medali ya shaba Olimpiki, alidhibitisha umahiri wake kama malkia wa mbio za 3000m kuruka viunzi na maji, akitetea taji lake kwa muda wa 8:57.24.
Akiwa amefunzwa na Bernard Rono katika kituo cha mazoezi cha Kalyet, Kericho, bingwa wa zamani wa dunia kwa vijana aliwashinda kwa ufasaha Norah Jeruto mwenye asili ya Kenya lakini anayewakilisha Kazakhstan (9:10.87), na Marwa Bouzayani wa Tunisia (9:12.03).
Kocha Rono alimpongeza akisema: “Tulikuwa na malengo, na taji la Diamond League lilikuwa shabaha kuu. Sasa tuna siku chache kurekebisha maandalizi yetu kabla ya mashindano ya Dunia.”
Mwanariadha Nelly Chepchirchir, anayefundishwa na gwiji wa mita 800 Janeth Jepkosgei, aling’aa katika mbio za mita 1500 wanawake, akipiga kasi ya ajabu katika raundi ya mwisho na kutwaa taji lake la kwanza la Diamond League.
Alikimbia kwa muda wa 3:56.99, baada ya kumpita Jess Hull wa Australia, aliyekuwa anaongoza mbio kwa muda mrefu lakini akalemewa mwishoni.
Vijana pia walionesha makali, ambapo Edmund Serem mwenye umri wa miaka 17, mdogo wake Amos Serem (bingwa wa Diamond League 2024), alionesha kina cha vipaji vya Kenya katika mbio za mita 3000 kuruka viunzi na maji.
Serem mdogo alikimbia 8:09.96, akinyakua fedha, nyuma kidogo ya Frederik Ruppert wa Ujerumani (8:09.02). Tayari akiwa sehemu ya kikosi cha Kenya kitakachoshiriki mashindano ya Dunia mjini Tokyo, kijana huyo alionesha yuko tayari kuwakabili wakali wa dunia.