News
Wanafunzi wa chuo kikuu cha Pwani wanataka uwazi kuhusu kifo cha Ojwang’
Baadhi ya wanafunzi wa chuo kikuu cha pwani mjini Kilifi kaunti ya Kilifi walijitokeza na kuilaumu serikali wakidai kwamba imezembea kulinda usalama wa raia wake kutokana na visa vya mauaji ya mara kwa mara dhidi ya raia.
Wakizungumza nje ya lango la chuo hicho wakiongozwa na Vincent Obondo wanafunzi hao waliitaka serikali kuwachukulia hatua maafisa wote wanaohusishwa na kifo cha Albert Ojwang’ mwanablogu ambaye alikuwa mwanafunzi wa chuo hicho.
Obondo pia alilaumu viongozi wa kisiasa nchini ambao wameonekana kunyamazia kisa hicho cha mauaji ya Ojwang wakisisitiza kujiuzulu kwa Naibu Inspekta Jenerali wa polisi Eliud Laga’t ili kupisha uchunguzi.
“Albert hakujigongesha kwa ukuta jinsi ambavyo polisi wenyewe wanasema, sasa tunauliza serikali ni nini ambayo vijana walifanya ambacho kinakufanya uwachukie hivi, kwa viongozi wetu kwa nini mmenyamaza sana hamjajitokeza waziwazi kuuliza serikali kwa nini wanafanya, tuko hapa kuuliza na kuagiza serikali kuchukua hatua kwa Eliud Laga’t aweze kujiuzulu pamoja na msemaji wa huduma ya kitaifa ya polisi”, walisema wanafunzi hao.

Wanafunzi wa chuo kikuu cha Pwani wakilalamikia mauaji ya Albert Ojwang’
Walidai lalama zote zinaelekezwa kwa Naibu Inspekta jenerali wa polisi Eliud Laga’t hivyo anapaswa kuwajibishwa wakidai hakuna uhuru wa kujieleza nchini na serikali imekuwa ikiendekeza udikteta na kunyamazisha wakosoaji wake.
“Hata hiyo nafasi heri ibaki wazi kuliko yule jamaa awe pale, kwa sababu nchi yetu haiwezi kuwa namna hii, sisi vijana tutajitokeza namna gani kuonyesha tuko salama au hatuko salama, Nasimama hapa nikiwa na wasiwasi sana kwa sababu sijui nitakujiwa lini lakini hatuogopi na ikifika mwaka 2027 tunaambia kila mtu kuwa unakuja kwa kituo cha kupigia kura na vitu viwili, kwanza kitambulisho cha kitaifa na pili akili yako timamu”, waliongeza wanafunzi hao.
Kwa upande wao Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu kaunti ya Kilifi wakiongozwa na Mwanase Ahmed, wameitaka serikali kuhakikisha maafisa wote wa polisi wanaohusishwa na visa vya mauaji ya raia kuwajibishwa.
“Sio mara ya kwanza kwa polisi kua wananchi hii kitu inaendelea na hakuna mtu ambaye amekamatwa na kufunguliwa mashtaka tangu mwaka jana, mimi nataka wachukuliwe hatua, tuko na jela, huu ni uhalifu dhidi ya binadamu”, aliongeza Mwanase.
Taarifa ya Joseph Jira