News

Wakaazi wa Voi waonywa dhidi ya ugonjwa wa MPOX

Published

on

Daktari wa magonjwa ya kuambukiza katika hospitali ya rufaa ya Moi mjini Voi katika kaunti ya Taita Taveta Urbanius Kioko amewataka wenyeji wa kaunti hiyo kuzingatia maagizo ya Wizara ya Afya ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.

Akiongea kwenye warsha ya Wanahabari iliyofadhiliwa na Shirika la Stawisha Pwani, Daktari Kioko alisema wananchi wanapaswa kujikinga ili kudhibiti ugonjwa huo kuenea.

Kioko pia aliwataka wale ambao wana dalili za ugonjwa huo kufika kwenye vituo vya afya ili kutibiwa.

“Huu ugonjwa huwa unaenezwa kupitia kutangamana, kuvaa nguo za mwenzako na kupitia hewa wakati wa kuongea’’, alisema Kioko.

Wadau wa sekta ya Afya katika kikao na Wanahabari mjini Voi

Vilevile, Kioko alitaja kisa cha mgonjwa mmoja wa Mpox kilichothibitishwa siku ya Jumanne wiki hii mjini Voi huku visa vingi vikishamiri katika kaunti Mombasa.

Haya yanajiri huku Wizara ya Afya nchini ikishinikiza wananchi kujiepusha kula nyama za Wanyamapori miongoni mwa tahadhari zingine kama njia mojawapo ya kukabiliana na maambukizi ya ugonjwa wa Mpox.

Taarifa ya Janet Mumbi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version