News
Wakulima Kilifi wanufaika na Ng’ombe wa maziwa.
Serikali ya kaunti ya Kilifi kupitia idara ya kilimo imeanzisha mpango wa kusambaza wa Ng’ombe wa maziwa kwa makundi ya wakulima wa mifugo kaunti hiyo.
Akizungumza na wanahabari wakati wa zoezi la ugavi wa ng’ombe hao eneo la Kakuyuni, waziri wa kilimo kaunti ya Kilifi Chula Mwagona alibainisha kuwa tayari jumla ya Ng’ombe 150 wamesambazwa katika maeneo mbalimbali ya kaunti hiyo kwa wafugaji.
Mwagona alikariri kuwa mradi huo unalenga kusambaza takriban ng’ombe 500 kwa makundi ya wafugaji ifikapo mwishoni mwa mpango huo.
“Kaunti ya kilifi idadi ya ng’ombe ambao tumesambaza inafika zaidi ya 150, kila kundi linapata ng’ombe 30 na saa hii tuko na makundi 17”, alisema Mwagona.
Wakati huo huo waziri huyo alidokeza kuwa mradi huo utapunguza pakubwa tatizo la uhaba wa maziwa ambao umekuwa ukikumba kaunti ya Kilifi mara kwa mara.
“Wakati kama huu uhaba wa maziwa umepunguwa kwa sababu maziwa yako kwa wingi, na kwa sababu sisi tumeanza kuwapatia wakulima ng’ombe tunatarajia kwamba ng’ombe wakianza kuzaa na kukamuliwa lile tatizo la maziwa ambalo tulikuwa tunapata litakuwa haliko”, aliongeza waziri huyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu