News
Wakaazi wa wakosoa kauli ya Rais Ruto dhidi ya viongozi wa kidini
Baadhi ya wakaazi kutoka kaunti ya Mombasa wamepinga matamshi ya Rais William Ruto kuwa viongozi wa kidini wamekuwa mstari wa mbele kuwachochea vijana dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza.
Kulingana na wakaazi, vijana wa kizazi cha Gen-z wamechukua hatua ya kuandaa maandamano ya mara kwa mara, kukemea vitendo viovu kupitia mitandao ya kijamii kutokana na hali ngumu ya maisha na ukosefu wa uwajibikaji miongoni mwa viongozi wakuu serikalini na wala sio viongozi wa kidini wamewachochea.
Wakaazi hao wamemtaka Rais Ruto kukubali kukosolewa na viongozi wa kidini kwani viongozi hao wamekua wakitekeleza wajibu wao wa kuikosoa serikali kwa njia ya Amani.
“Kusema kweli ni kama Rais hataki kukosolewa kwa sababu hawa viongozi wanafanya kazi yao na wamekua wakifanya hivyo hata kwa serikali zilizopita na kama wewe mtu hutaki kukosolewa itakuwaje?” … aliuliza mmoja wa wakaazi.
Wakaazi hao aidha wameshikilia kuwa kando na viongozi wa kidini wao pia kama wananchi wana haki ya kuikosoa serikali kwani ni jukumu lao kikatiba huku wakiapa kutonyamazia madhila yanayotekelezwa na viongozi.
Taarifa ya Elizabeth Mwende