News
Vijana wahimizwa kuepuka mihadarati
Vijana wamehimizwa kujitenga na matumizi ya dawa za kulevya kutokana na athari zake ambazo zimechangia maisha ya vijana wengi kusambaratika.
Hii ni baada ya Mamlaka ya kukabiliana na mihadarati na vileo haramu nchini Nacada kubaini ongezeko la idadi ya vijana katika uraibu huo.
Akizungumza katika shule ya upili ya wavulana ya Malindi high katika kaunti ya Kilifi, mkurugenzi wa Wakfu wa Smachs-Charlene Ruto alisema vijana wana jukumu kubwa la kuchukua mwongozo wa maisha yao na wala sio kulaumu viongozi.
“Fukuza dawa za kulevya, karibisha mabadiliko, huu ndio ujumbe pekee tuliokuja kuwapa leo, vijana, asilimia 70 ya uongozi unaanza na wewe mwenyewe, tunapenda kuelekeza lawama kwa serikali ni mwalimu au mzazi, lakini kama vijana tuchukue jukumu na mabadiliko yanaanza na sisi wenyewe”,alisema Charlene Ruto.
Kwa upande wake Rais wa Muungano wa wanafunzi kaunti Kilifi Kahindi James Kalama alisema kaunti ya Kilifi ina vijana wengi ambao ni waraibu wa dawa za kulevya jambo ambalo linafaa kuangaziwa kwa kina, kauli ambayo iliungwa mkono na rais wa Jumuiya ya wanafunzi wa Pwani David Msongori.
“Kilifi inaidadi kubwa ya vijana ambao wameathirika na matumizi ya dawa za kulevya, tukifuata takwimu za Nacada na ndio maana tumekuja na kongamano kama hili ambao tuko nalo siku ya leo kuhamasisha athari ya mihadarati ili waweze kuachana nayo na kufuata elimu”, alisema Kalama.
Kwa upande wake naibu gavana wa kaunti ya Kilifi Flora Mbetsa Chibule aliwahimiza wanafunzi kuzingatia masomo yao ili kubadili msimamo wa maisha yao badala ya kujiingiza katika mambo yasiofaa.
“Mbali na kwamba tunafukuza dawa za kulevya eneo letu, nyinyi wanakilifi leo na vijana wote nchini tunasema tunawatambua na serikali inaimani na nyinyi.”, alisema Chibule.
Baadhi ya viongozi wa mashirika walioandamana na mwanawe rais William Ruto walisema matumizi ya dawa za kulevya yamesambaratisha maisha ya vijana wengi ambao wamekosa mwelekeo maishani, wakiwarai viongozi wa kaunti kuweka mikakati ya kunusuru maisha ya vijana hao.
Taarifa ya Joseph Jira