Mshikilizi wa Rekodi mpya mbio za masafa marefu Sebastian Sawe anasema ushindi wake unamuendea bingwa wa zamani marehemu Kelvin Kiptum

Mshikilizi wa Rekodi mpya mbio za masafa marefu Sebastian Sawe anasema ushindi wake unamuendea bingwa wa zamani marehemu Kelvin Kiptum

Mshikilizi wa rekodi ya dunia ya marathon, Sebastien Sawe, amesema ushindi wake wa Jumapili katika Marathon ya London ambapo aliweka rekodi mpya ya dunia ya marathon anautoa kwa ajili ya marehemu Kelvin Kiptum aliyefariki Februari 2024 katika ajali mbaya ya barabarani.

Akizungumza baada ya kuvunja rekodi ya marathon katika Marathon ya London kwa muda wa saa 1 dakika 59 na sekunde 30, Sawe alisema Kiptum alikuwa mfano wa kuigwa kwa wengi na alimpa msukumo wa kukimbia.

“Yeye [Kelvin Kiptum] aliwahamasisha wengi kufanya kazi kwa bidii na kuvunja rekodi. Kutokana na bidii aliyoweka na nidhamu aliyokuwa nayo, nina hakika anajivunia kile nilichofanikisha,” alisema Sawe.

Sawe alikuwa amelenga kuvunja rekodi ya dunia ya Kiptum huko Berlin Septemba mwaka jana, alipofika nusu ya mbio kwa dakika 60:16, kabla juhudi hiyo kuvurugwa na hali ya hewa ya joto kali.

Sasa anasema ushindi wa Jumapili ulitokana na bidii na kujitolea.

“…Matokeo ni zao la kazi ngumu niliyoweka katika mazoezi; si rahisi, lakini kupitia nidhamu na kujitolea ndoto imetimia,” aliongeza Sawe.

Sawe, anayeshikilia rekodi na ambaye ameshinda marathoni zote nne alizoshiriki, amejitahidi kudumisha uaminifu katika mafanikio yake kwa kufanyiwa vipimo vya mara kwa mara vya dawa zilizopigwa marufuku, na alipimwa mara 25 kabla ya kushiriki Berlin, ambako alishuka kasi na kumaliza kwa muda wa 2:02:16.

“Nimekumbana na majeraha kadhaa lakini hayakunifanya niache ndoto yangu. Ninafurahi kuwa imetimia na ninaamini zaidi yatakuja siku zijazo,” alisema mshikilizi huyo wa rekodi ya dunia ya marathon.