Mkufunzi wa klabu ya Mancity Pep Guardiola ameisifia mafanikio yao ya kuwa timu ya kwanza kufika fainali nne mfululizo za FA Cup baada ya kurejea kwa nguvu mwishoni na kuinyima Southampton ushindi wa kushtukiza katika uwanja wa Wembley.
Klabu ya Southampton walikuwa wakielekea kufuzu kwa fainali yao ya kwanza baada ya miaka 23 wakati Finn Azaz alipofunga bao zuri na kuipa timu hiyo ya Championship uongozi dakika 11 kabla ya muda kuisha.
Hata hivyo, City walisawazisha haraka kupitia kwa Jeremy Doku kabla ya Nico Gonzalez kufunga bao la kuvutia na kuwapa ushindi wa 2-1 katika nusu fainali hiyo.
Kikosi cha Guardiola kimepoteza fainali mbili zilizopita za FA Cup dhidi ya Crystal Palace na Manchester United, huku wakiwashinda Manchester United mwaka 2023.
City, ambao watakutana na Chelsea katika fainali, sasa wako kwenye nafasi nzuri ya kushinda mataji matatu ya ndani.
Wachezaji wa Guardiola walitwaa Kombe la Ligi mwezi uliopita na kwa sasa wako kwenye ushindani mkali wa ubingwa wa Ligi Kuu dhidi ya Arsenal.
“Hakuna timu iliyofika fainali nne mfululizo. Ni jambo la ajabu na tunatumaini tutafika tukiwa na kasi nzuri,” alisema Guardiola.
Uamuzi wa kocha wa City kufanya mabadiliko nane kutoka kikosi kilichoishinda Burnley 1-0 Jumatano ulionekana kuwa wa kutiliwa shaka, huku Southampton wakitawala kipindi cha kwanza.
Hata hivyo, kikosi cha Guardiola kiliboresha mchezo wao sana baada ya mapumziko na kusaidiwa na kuingia kwa Doku, Erling Haaland na Bernardo Silva kutoka benchi.
“Ilikuwa ngumu lakini winga (Doku na Savinho) walipoingia walibadilisha kasi ya mchezo,” aliongeza Guardiola.
“Mara ya kwanza walipovuka mstari wa katikati walitengeneza bao la kushangaza. Soka huwa halitabiriki lakini namna tulivyocheza kipindi cha pili ilikuwa ya kipekee.”
