Mwakilishi wa Soka la Wanawake Kaunti ya Kilifi, Elizabeth Santa Hinzano, amesema kuwa mwaka jana shirikisho lilijitahidi kuweka mikakati ya kuanzisha Ligi ya Wanawake ya Kaunti.
Hinzano ameeleza kuwa FKF Kilifi ilichukua hatua madhubuti ikiwemo kupunguza ada ya ushiriki kwa asilimia 50 ili kuvutia timu nyingi zaidi kushiriki katika ligi hiyo.
“Hata hivyo, hadi kufikia mwisho wa msimu, hakuna hata timu moja iliyojitokeza kushiriki ligi ya wanawake,” alisema Hinzano kwa masikitiko.
Amesisitiza kuwa hali hiyo haiwezi kuendelea mwaka huu, akiahidi kuwa ni lazima ligi ya akina dada ianzishwe ndani ya Kaunti ya Kilifi.
“Mwaka huu hatutakubali soka la wanawake kubaki nyuma. Ni lazima tuanzishe ligi ya akina dada hapa Kilifi,Kama FKF Kilifi, msimu huu tumeipa kipaumbele cha juu soka la wanawake,” aliongeza.
Hinzano ametoa wito kwa vilabu, wadau na wazazi kuwaunga mkono wasichana wenye vipaji ili kuwapa fursa ya kuonyesha uwezo wao na kukuza soka la wanawake katika kaunti hiyo.
