Serikali ya kaunti ya Kilifi imefutilia mbali baadhi ya miradi iliyokwama ambayo ilikuwa imekabidhiwa Wanakandarasi na kushindwa kuitekeleza.
Hii ni baada ya Mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali Nancy Gathungu kuagiza zaidi ya kaunti 20 nchini zilizoshindwa kusimamia vyema fedha na raslimali za umma kutopewa mgao mwengine wa fedha na serikali ya kitaifa.
Kaunti hizi zinadaiwa kutotumia raslimali za umma vyema hasa wakati wa bajeti ya mwaka wa kifedha wa awali na kuchangia ofisi ya mkaguzi wa hesabu za serikali kutoa taarifa hiyo kwa umma.
Katika kikao na Wanahabari, Gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro alisema baadhi ya miradi ambayo imefutiliwa mbali ni ile ya barabara za mashinani, ujenzi wa shule za Chekechea miongoni mwa miradi mingine, akisema miradi hiyo sasa itakabidhiwa wananchi kuikamilisha.
“Tumesema miradi ile ambayo wanandarasi walipewa na kaunti na wameshindwa kuitekeleza, hiyo iimefutiliwa mbali na wananchi sasa watapewa nafasi kuitekeleza, haiwezekana umepewa kazi ufanye alafu unashindwa wakati wananchi wanataka hiyo miradi kunufaika”, alisema Mung’aro.
Gavana Mung’aro alishikilia wanakandarasi waliopewa zabuni na kushindwa kuikamilisha miradi ya kaunti hawatalipwa fedha zao na miradi hiyo kukabudhiwa wanakandarasi wengine.
Akigusia suala la bills ambazo hazijalipwa, Gavana Mung’aro alidokeza kwamba kamati maalum itabuniwa ili kufuatilia suala hilo sawa na kutatua changamoto zilizopo.
Taarifa ya Mwahoka Mtsumi
