Akizungumza baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa FKF tawi la Kilifi, Dickson Angore, alisema kuwa maandalizi yote yamekamilika ili kuhakikisha msimu huu unafanyika kwa mafanikio.
“Tumefanya mkutano na vilabu na matumaini yetu ni kwamba ligi itaanza mwezi ujao, Mungu akipenda, kwani tayari imechelewa kuanza. Lengo letu ni kuhakikisha kila kitu kiko sawa kabla ya kipenga cha kwanza,” alisema Angore.
Katika kikao maalum kilichowahusisha wakufunzi na wasimamizi wa vilabu mjini Kilifi, ilikubaliwa kuwa baada ya makubaliano kuhusu ada za usajili na ushiriki, pamoja na vilabu kutimiza wajibu wao wa kifedha, ligi hiyo itafunguliwa rasmi.
“Tunatarajia vilabu vitawajibika kulipa ada kwa wakati ili tuanze mchakato wa usajili na utengenezaji wa kadi za wachezaji, jambo litakalowezesha ligi kuanza bila vikwazo,” aliongeza mwenyekiti huyo.
Angore pia alithibitisha kuwa kozi za ukocha zitaanza ndani ya wiki mbili zijazo, akitoa shukrani kwa Wizara ya Michezo ya Kaunti ya Kilifi kwa ushirikiano wake na shirikisho hilo.
“Tumewasilisha mipango yetu kwa kaunti na makocha wako tayari. Tunatarajia ndani ya wiki mbili zijazo mafunzo hayo yaanze rasmi. Aidha, tunaendelea na mazungumzo na ofisi ya kitaifa ili tuongeze darasa lingine kwa kuwa lililopo halitoshelezi mahitaji,” alisema.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa FKF tawi la Kilifi, Odak Onyango, alisisitiza umuhimu wa nidhamu na uwajibikaji kutoka kwa vilabu, hasa katika kufuata ratiba ya mechi.
“Ratiba itatolewa mara tu vilabu vitakapokamilisha malipo ya ada ya ushiriki. Naomba vilabu vizingatie ratiba kikamilifu ili kuepusha sababu za kuahirisha mechi tena,” alieleza Onyango.
Naye Mwakilishi wa Wanawake wa FKF Kilifi, Elizabeth Hinzano, alieleza masikitiko yake kuhusu kushuka kwa kiwango cha soka la wanawake kaunti humo, akiahidi kuchukua hatua za kulifufua.
“Inasikitisha kuona soka la wanawake likidorora kwa sababu wengi hawajawa tayari kujihusisha nalo. Hata hivyo, nina imani kwamba chini ya uongozi wangu tutaleta mwamko mpya. Ninalenga kuwawezesha wasichana na kuwasaidia kujenga taaluma katika ukocha na uongozi wa soka,” alisema Hinzano.
Jumla ya vilabu 74 vilihudhuria mkutano huo, vikionesha nia ya kushiriki katika Ligi Kuu ya Kaunti ya Kilifi msimu huu.
