Bingwa wa toleo la 35 la mbio za Discovery Cross Country zilizofanyika Eldoret, kaunti ya Uasin Gishu, Maryam Lufti Njoki, anatarajiwa kurejea katika mashindano ya Sirikwa Classic Cross Country yatakayofanyika Jumamosi, Februari 14, mwaka huu katika kijiji cha Lobo, Kapseret akilenga kuboresha nafasi yake baada ya kumaliza wa 12 mwaka 2023 aliposhiriki kwa mara ya mwisho katika uwanja huo.
Njoki, ambaye awali alijulikana kama Christine Njoki kabla ya kubadili uraia na kuwakilisha Qatar, amesema kurejea kwake kunachochewa na nia ya kupata matokeo bora zaidi huku akiendelea kujiandaa kwa msimu wa mashindano ya uwanjani akisema ana uzoefu zaidi sasa na ana matumaini ya kuonyesha kiwango cha juu dhidi ya wapinzani wake.
Katika kitengo cha wanawake, Njoki atakumbana na ushindani mkali kutoka kwa bingwa wa dunia wa mbio za nyika Agnes Jebet Ng’etich pamoja na mshindi wa medali ya fedha ya dunia kutoka Uganda, Joy Cheptoyek.
Wengine watakaoshiriki ni pamoja na Catherine Reline ambaye sasa anawakilisha Uturuki kwa jina la Can, wanariadha wengine kutoka Uganda na Tanzania pia wanatarajiwa kushiriki katika mbio za kilomita 10 kwa wanawake.
Kwa upande wa wanaume, Mjerumani Hendrik Pfeiffer atarejea kushiriki mashindano hayo, Mykola Nyzhnyk wa Ukraine, Tshepo Mphulanyane wa Afrika Kusini na Leonard Ndiema wa Uganda miongoni mwa washindani wa kimataifa.
Mashindano hayo yanatarajiwa kuwa ya ushindani mkubwa huku wanariadha wakitumia kama sehemu ya maandalizi ya mashindano makubwa yajayo.
