National News
Shahidi wa 28 na 29 Waelezea Mahakama Masaibu Waliyopitia Shakahola
Kesi inayomhusu Mhubiri tata Paul Mackenzie na wenzake 92 imesikizwa katika Mahakama ya Mombasa, ambapo shahidi wa 28 na 29 wameeleza ushahidi wao Mahakamani.
Shahidi wa 28, ambaye ni mtoto ametoa ushahidi wake katika chumba cha faraga ambapo amesema kwamba alikamatwa na maafisa wa polisi pamoja na familia yake baada ya wazazi wake kuwaachisha shule kutokana na mafunzo ya Mackenzie.
Mtoto huyo ameeleza kwamba baba yake alikuwa akipinga mafunzo ya Mackenzie lakini baadaye alijiunga na kisha kuhamia Shakahola na familia yake ambapo alishuhudia Mackenzie akikusanya watu na kuwaagiza kufunga kula na kunywa, kabla ya kufanikiwa kutoroka hadi kituo cha watoto huko Watamu.
Kwa upande wake Shahidi wa 29, ameiambia Mahakama hiyo kwamba alipoteza watoto wake 7 kutokana na kufunga kula na kunywa, akisema walinzi waliokuwa wakilinda eneo hilo walichukua chakula chake chote kilichokuwa nyumbani kwao.
Shahidi huyo amesema wakati huo alikuwa mjamzito na alilazimika kufunga ili kuua mtoto aliyekuwa tumboni na wafuasi wa Mackenzie walikuwa hawaruhusiwi kuomboleza kifo chochote katika eneo hilo la Shakahola.
Mackenzie na wenzake 92 wanakabiliwa na mashtaka 238 ikiwemo mauaji ya halaiki, ugaidi, mafunzo ya itikadi kali miongoni mwa mashtaka mengine yanayodaiwa kuyatekeleza kati ya mwaka 2020 na 2023 katika msitu wa Shakahola kaunti ya Kilifi.
Kesi hiyo inaendelea kusikilizwa mbele ya Hakimu mkuu Alex Ithuku.