News

Polisi wasimamishwa kazi kwa kumpiga risasi mchuuzi.

Published

on

Huduma ya kitaifa ya polisi NPS imewasimamisha kazi maafisa wawili wa polisi wanaohusishwa na kisa cha kupigwa risasi raia ambaye hakuwa na silaha wakati maandamano ya kushinikiza naibu inspekta jenerali wa polisi Eliud Lagat kujiuzulu siku ya jumanne 17, Juni 2025 jijini Nairobi.

Maafisa hao wawili hao, Konstebo Klinzy Barasa Masinde na Duncan Kiprono, walinaswa katika video ambayo sasa inasambaa mitandaoni ikionyesha afisa mmoja akimpiga risasi mchuuzi wa barakoa, na kumwacha akidhania kuwa amefariki kwenye barabara ya Moi Avenue jijini Nairobi.

“Maafisa hao wawili sasa wamesimamishwa kazi na wanashughulikiwa na kitengo cha maafisa wa kukabiliana na mauaji, makao makuu ya maafisa wa upelelezi wa makosa ya jinai-DCI, wakisubiri hatua zaidi,” ilisoma taarifa hiyo iliyotiwa saini na msemaji wa NPS Muchiri Nyaga.

Huduma ya polisi iliongeza kuwa mwanamme aliyejeruhiwa, hali yake ya afya inaendelea vyema katika hospitali ya kitaifa ya Kenyatta jijini Nairobi baada ya kufanyiwa upasuaji.

“Huduma ya kitaifa ya polisi NPS inajutia sana kitendo hiki kisicho na msingi na inamuhurumia mwathiriwa na familia yake, huku ikisisitiza kujitolea kwake kikamilifu kuhakikisha haki inatendeka,” iliongeza taarifa hiyo.

Hatua ya kuwatambua maafisa hao ilitokana na lalama za wananchi kushinikiza  huduma ya polisi nchini kubaini waliohusika katika kosa hilo.

Maandamano hayo yaliyomtaka naibu inspekta jenerali wa polisi Eliud Lagat ajiuzulu, yaligeuka na kuwa machafuko baada ya wahuni kuingilia kati na kutatiza waandamanaji.

Katika mojawapo ya video ambazo zilizua taharuki kwa umma, maafisa hao walimkabili mchuuzi huyo wa barakoa ambaye hakuwa na silaha kabla ya mmoja wao kufyatua risasi akiwa karibu.

Taarifa ya Joseph Jira

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version