News

Panda shuka za kiuongozi katika serikali za ugatuzi

Published

on

Huku Kongamano la Ugatuzi awamu ya 12 likiendelea kaunti ya Homa Bay, bado Wakenya wanaendelea kutathmini iwapo malengo ya ugatuzi yanatimizwa.

Yapo maswali mengi tu kuhusu ufanisi wa kimaendeleo na utenda kazi wa serikali za kaunti ambazo hadi sasa nyingi zao zinazidi kulaumiwa kwa kuendeleza ufisadi, usimamizi mbaya wa rasilimali, na utoaji wa huduma duni, suala ambalo limeendelea kuwamulika magavana na maafisa wengine wa serikali za kaunti.

Tangu Ugatuzi uanzishwe baada ya katiba mpya ya mwaka 2010, Bunge la seneti limetenga takribani shilingi trillioni 4 kwa serikali za ugatuzi kupitia mfumo wa ugavi wa rasilimali za serikali kwa huduma za kaunti, ingawa bado kuna maswali mengi kuliko majibu kuhusu malengo yaliyokusudiwa sheria hii ya ugatuzi.

Uongozi wa serikali hizi bado upo kwenye mizani na mitihani mingi tu, ikiwa ni pamoja na ahadi nyingi zinazotolewa na viongozi wa serikali hizi za kaunti ambazo hazitimizwi kutokana na kile wananchi wanadai ni ukiritimba unaotokana na uongozi mbaya, ufisadi na upendeleo katika utoaji wa huduma na kandarasi.

Suala la utoaji wa kandarasi limekuwa donda sugu katika serikali nyingi za kaunti, huku zikiendelea kukabiliwa na malimbikizi ya madeni.
Miongoni mwa sekta zinazotajwa kuathirika zaidi na usimamizi mbaya au ufujaji wa pesa za umma ni sekta ya afya ambayo. Hospitali nyingi hazina dawa huku huduma za afya zikiendelea kudorora kuanzia ngazi za zahanati hadi hospitali kubwa za kaunti.

Serikali za kaunti pia zinashtumiwa kwa kuendelea na uratibu wa miradi hewa katika bajeti zao, na kupelekea kupotea kwa mabilioni ya pesa za uma.

Japo Ugatuzi ulilenga kuboresha maisha ya Wananchi katika ngazi za chini, bado umaskini umekithiri huku mizozo ya uongozi na utawala wa kibepari vikiendelea kushuhudiwa kati ya mabunge ya kaunti na ofisi za magavana.

Wanawake wakichota maji kutokana na manufaa ya ugatuzi {picha kwa hisani}

Matokeo ya mizozo hiyo mara nyingi yamekuwa kushuhudiwa kwa mapinduzi katika usimamizi wa ofisi za magavana kupitia hoja za kutokuwa na Imani nazo, au kutokuwa na Imani na usimamizi wa mabunge ya kaunti na Maspika wa mabunge hayo, hatma yake ikiwa ni kushinikizwa kutimuliwa kutoka ofisi zao.

Taarifa ya Eric Ponda

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Trending

Exit mobile version