Kanja: Polisi kuwasaka mawakala tapeli wa ajira za ughaibuni

Kanja: Polisi kuwasaka mawakala tapeli wa ajira za ughaibuni

Inspekta Jenerali wa Polisi nchini Douglas Kanja amesema uchunguzi unaendelea ili kuwatambua mawakala matapeli waliowahadaa wakenya kujiunga na jeshi la Urusi kupigana vita dhidi ya Ukraine.

Akizungumza mjini Mombasa katika Kongamano la usalama, Kanja alisema maafisa wa Idara ya upelelezi wa makosa ya Jinai, DCI, tayari wameanzisha uchunguzi wa kina kuhusu sakata hiyo.

Aidha alionya kwamba yeyote atakayepatikana na hatia atachukuliwa hatua kali za kisheria na kufikishwa Mahakamani, akieleza wasiwasi wake kuhusu ongezeko la visa vya uhalifu vinavyohusishi baadhi ya wahudumu wa bodaboda.

Afisa huyo mkuu wa polisi nchini aliwataka wahudumu badoboda kujisajili katika makundi au vyama vinavyotambulika kisheria ili kurahisisha utambuzi wao na kudhibiti wale wanaotumia sekta hiyo kama kisingizio cha kutekeleza uhalifu.

Aidha, aliwaonya vijana wanaojihusisha na magenge ya kihalifu maarufu kama Panga boys, akisisitiza kuwa Jeshi la Polisi halitavumilia vitendo vya aina hiyo.

Wakati huo huo alisema kwamba maafisa wa usalama watachukua hatua madhubuti dhidi ya wahalifu wote ili kulinda maisha na mali ya wananchi.

Kanda na hayo, Afisa huyo wa mkuu wa polisi aliongeza kwamba kadri taifa linajiandaa kwa uchaguzi mkuu, vyombo vya usalama vinaendelea kubuni na kuimarisha mikakati ya kuhakikisha taifa linashuhudia amani, utulivu na usalama.

Taarifa ya Mwanahabari wetu