Kamishna wa kaunti ya Mombasa Mohamed Noor amewahakikishia wakaazi wa Mombasa usalama wa kutosha msimu huu wa mwezi mtukufu wa Ramadhan kwa waislamu pamoja na mfungo wa Kwaresma kwa wakristo.
Akizungumza na Wanahabari, Noor alisema kamati ya usalama kupitia Kamanda mkuu wa polisi eneo hilo imeweka mikakati thabiti kuhakikisha usalama unaimarishwa.
Noor alisema ratiba za maafisa wa usalama kushika doria za usiku na mchana imepangwa ili kuhakikisha maafisa wa usalama wa kutosha wanakuwa nyanjani kukabiliana na visa vyovyote vya utovu wa usalama.
Noor alitoa onyo kali kwa wale wote wanaonuia kufanya uhalifu, akisema kuwa watachukuliwa hatua kali za kisheria.
“Tumetoa onyo kwa watu ambao wanalenga kutekeleza uhalifu kwamba wakome ama watakabiliwa na mkono wa sheria”, alisema Noor.
Ni kauli iliyopigiwa upatu na Sheikh Juma Ngao ambaye amesema waislamu watakuwa wakifanya ibada za usiku jambo ambalo limepelekea shinikizo zake za kuitaka idara ya usalama kuwajibika vilivyo.
Taarifa ya Mwanahabari wetu
