Mahakama ya Kilifi imemnyima dhamana mwanaume mmoja anayekabiliwa na shtaka la unajisi wa mtoto wa umri wa miaka 11 kisha kutishia kumuua iwapo angesema kuhusu kitendo hicho.
Hakimu wa Mahakama hiyo Ivy Wasike aliagiza kuzuiliwa rumande kwa mshukiwa huyo Hamis Bakari Karisa baada ya kiongozi wa mashtaka Nancy Njeru kueleza Mahakama kwamba mshukiwa huyo ana kesi yengine ya kujibu ya unajisi katika Mahakama hiyo iliyowasilishwa mbele ya Hakimu Charles Obulutsa.
Vile vile kiongozi wa mashtaka alieleza Mahakama kwamba mshukiwa alitekeleza kitendo hicho cha unajisi baada ya kuachiliwa kwa dhamana kwa kesi awali aliyokuwa ikimkabili ya unajisi ambayo bado inaendelea.
Awali Mahakama ilielezwa kwamba mshtakiwa alitekeleza kitendo hicho cha unyama siku tofauti kati ya tarehe 23 hadi 29 mwezi Septemba mwaka 2025 eneo la Tezo kaunti ya Kilifi.
Hata hivyo Mahakama iliagiza mshukiwa kurudishwa Mahakamani mnamo tarehe 20 mwezi Novemba mwaka 2025 ambapo kesi hiyo itasikizwa mbele ya Hakimu James Mwaniki
Taarifa ya Teclar Yeri