Rais William Ruto amesisitiza kuwa serikali yake inawekeza kwa kiwango kikubwa katika sekta muhimu za elimu na afya ili kuhakikisha maisha bora kwa wananchi.
Akizungumza katika Chuo Kikuu cha Umma, kaunti ya Kajiado, Rais Ruto alisema serikali imeongeza mgao wa fedha kwa vyuo vikuu kwa zaidi ya shilingi bilioni 130 ili kuinua kiwango cha elimu ya juu nchini. Alibainisha kuwa hatua hiyo inalenga kusaidia wanafunzi wengi zaidi kupata nafasi ya masomo na kuboresha ubora wa elimu.
Ruto aliongeza kuwa wanafunzi takriban 470 tayari wamenufaika na ufadhili na mikopo ya elimu kutoka serikali ya kitaifa. Aidha, alieleza kuwa vyuo vya kiufundi vimeimarika kwa kiwango kikubwa, na kupitia hamasa zinazofanyika kote nchini, idadi ya wanafunzi wanaojiunga na taasisi hizo imeongezeka maradufu. Rais alisema wanafunzi hao wanajipatia ujuzi muhimu utakaowasaidia kujiajiri na kukuza uchumi wa taifa siku zijazo.

Viongozi wahudhuri mkutano wa masuala ya elimu na afya uliogongwa na Rais William Ruto{Picha kwa hisani}
Kwa upande wake, Waziri wa Afya Aden Duale aliunga mkono kauli ya Rais akisisitiza kuwa serikali imepiga hatua kubwa katika mageuzi ya sekta ya afya. Duale alisema zaidi ya Wakenya milioni 26.5 tayari wamejiandikisha na Bima ya Afya ya Jamii (SHA) na kunufaika nayo, ikilinganishwa na milioni 7 pekee waliokuwa kwenye NHIF.
Waziri huyo alifafanua kuwa bima ya NHIF iliacha deni kubwa na haikuwajumuisha wananchi wote, tofauti na SHA inayolenga kila Mkenya. Duale pia aliwataka viongozi wa kisiasa kukoma kuingiza siasa katika sekta muhimu kama afya na elimu na badala yake kushirikiana na serikali katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora.
Taarifa ya Elizabeth Mwende